Na JUSTIN DAMIAN,
BIASHARA ya nyumba na ardhi zipo katika hali mbaya. Wadau katika sekta hii wanasema, kipindi cha mwaka 2016 mpaka hivi sasa, kinaendelea kuwa ni kipindi kibaya zaidi.
Kwa kipindi cha miaka kadhaa, sekta ya nyumba imekuwa ikifurahia ukuaji mzuri na wakuridhisha.
Hali hii inathibitishwa na ujenzi wa majengo ya biashara na nyumba za kuishi karibu kila kona ya nchi.
Kwa ujumla wake, sekta ya ujenzi wa majengo ya biashara na makazi katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 imeshuhudia ukuaji mzuri wa wastani wa asilimia 23.2.
Hata hivyo, mwelekeo huo ulibadilika ghafla mwaka jana ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka, ukuaji wa sekta hiyo ulikuwa ni asilimia 4.3. Hii ni kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini sekta hizi mbili zipo katika wakati mgumu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ngumu ya kiuchumi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanganyika Estate Agents Limited yenye makao yake jijini Arusha, Donald Lema, anasema biashara hiyo imezorota kwa kiasi kikubwa jijini Arusha.
Kampuni ya Lema inajishughulisha na kupangisha nyumba, ofisi pamoja na kuuza ardhi na nyumba.
“Katika upangishaji kuna upungufu mkubwa sana wa wateja, wateja wengi wameondoka, pili ni kuwa, uwezo wa wateja kifedha umepungua.
“Hapa Arusha tulikuwa tuna watu kama 1,000 kwenye soko la nyumba. Watu hawa ni wale waliokuwa wakifanya kazi katika Hahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambao hawapo kwa kuwa shughuli za Mahakama hiyo zimemalizika,” anasema Lema
Anasema kwa sasa taasisi ambazo zinategemewa katika soko la nyumba ni wale Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lakini anasema Jumuiya hiyo haina watu wengi na watu wake uwezo wao ni wakawaida.
“Watu wengine ni mahakama ya Afrika ambao pia ni wachache na uwezo wao ni kama wa watu wa EAC, wastani wa Dola za Kimarekani 400 kwa mwezi.
“Wengine ni wamisionari pamoja na wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa ambao ni wachache sana. Mpaka sasa hivi hatujapata wateja ambao wanaweza kuziba pengo la hao 1,000 waliondoka,” anafafanua.
Anaendelea kusema “hii manake ni kuwa, nyumba ni nyingi kuliko mahitaji na hivyo bei za nyumba zimeshuka sana. Mtu anakaa na nyumba kwa zaidi ya miezi mitatu bila mpangaji, mwisho anaona bora apangishe kwa bei ambayo mteja anatoa kuliko kuendelea kukaa nayo tu.
“Nyumba ambayo ilikuwa inapangishwa kwa dola 800 imeanguka kwa asilimia 30, kwa sasa unaweza kuipata kwa Dola 500 mpaka 450. Tatizo lingine tofauti na kipindi cha nyuma, mteja anapoleta nyumba kwetu ili tumtafutie mteja haitoki haraka, inaweza kukaa hata zaidi ya miezi mitatu bila kutoka,” anasema.
Anasema, “uwezo wa kupangisha umeshuka kiasi kwamba wanawashauri wenye nyumba kujenga nyumba ndogo ndogo za gharama ya kuanzia Sh 200,000 mpaka 250,000.
“Kingine tunawashauri kuchukua kodi ya mwezi mmoja hadi mitatu na siyo zaidi, mambo ya miezi sita kwa sasa yamekuwa magumu,” alisema.
Lema anasema kwenye ardhi hali ni mbaya zaidi. “Nataka nikuhakikishie kuanzia Fourth of January (Januari nne) mpaka sasa hakuna mteja hata mmoja ambaye amekuja japo kuulizia tu kuhusiana na ardhi,” anasema.
Mkurugenzi huyo anasema kipindi kabla ya uchaguzi, mtu alikuwa anaweza kutoa tangazo la ardhi kupitia tovuti ya kampuni yake na ndani ya siku mbili akalipa tena kwa fedha taslimu.
“Kwa ujumla hali ilikuwa ni nzuri. Pamoja na kuwa bei zilikuwa juu watu walinunua kwa wingi,” anafafanua.
Anasema wateja wake wengi walikuwa ni watumishi wa umma ambao mara nyingi wanapokuwa wananunua ardhi, hupenda kuficha utambulisho wao lakini kwa kuwa walikuwa hawana matatizo kwenye kulipa hilo halikuwa tatizo kwake.
Katika kipindi hicho, tulikuwa tunapata wateja wanaoulizia zaidi ya kumi kwa mwezi na tuliweza kufanya biashara mbili, tatu au hata zaidi. Lakini kwa sasa hata wa kuulizia hayupo,” anasema
Akizungumzia majengo yanayopangisha nafasi za ofisi anasema nako pia hali si nzuri. Lema anaeleza kuwa, kipindi cha nyuma makampuni ya utalii yalikuwa wateja wazuri lakini kutokana na maendeleo ya teknalojia, makampuni mengi yanafanya kazi kutokea majumbani
“Mara nyingi utakuta nyumba ya kuishi chumba kimoja kinageuzwa ofisi ili mradi tu kuna huduma ya mtandao. Kampuni nyingi za utalii hazihitaji kuwapeleka wageni wake ofisini, wakiwachukua uwanja wa ndege wanawapeleka hotelini na kama ni briefing inafanyikia hapa kisha wanapekekwa sehemu wanazokwenda kutembelea,” anasema Lema.
Akitolea mfano wa Mafao House ambalo ni jengo la ghorofa saba ambalo kampuni yake inalitafutia wateja, anasema bado linachangamoto ya kupata wateja wa kutosha.
“Ghorofa ya chini imejaa, ghorofa ya kwanza na ya pili wapo wenyewe ila kuelekea huko juu kupo wazi. PPF Tower ambayo lipo mkabala na Kibo Palace Hotel ni kama haina wapangaji kabisa. Bei pia zinashuka sana, kwa mfano Mafao House ni dola 9 kwa skwea mita ikiwa ni pamoja na usafi, ulinzi na AC (kiyoyozi).
“Ukitoa gharama hizo utakuta ni kama dola sita kwa skwea mita. Kipindi cha nyuma jengo kama AICC walikuwa wanatoza mpaka dola 25 kwa skwea mita,” anase,a.
John Butimali ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Seven Estate Agency ya jijini Dar es Salaam, naye anasema upepo wa biashara umebadilika kwa kasi kubwa.
“Mwaka juzi (2015) mwezi wa saba kurudi nyuma nilikuwa nikipokea barua pepe (e-mail) 40 mpaka 50 za wateja ambao walikuwa wakitaka kununu nyumba, viwanja.
“Kwa sasa hali imebadilika, kwa siku napokea barua pepe tatu au nne na wateja hao utakuta wanaulizia nyumba za bei nafuu kati ya Sh milioni 70 hadi 120.
“Kipindi hicho, biashara ya Dola za Marekani 500,000 hadi milioni moja ilikuwa ni jambo la kawaida kukutana nazo katika shughuli zetu. Ukweli biashara ya nyumba imeporomoka sana kwa sasa, wateja tuliokuwa tunawategemea hawapo tena,” anasema.
Naye Jonas Alias ambaye ni dalali maarufu wa nyumba na viwanja eneo la Sinza, jijini Dar es Salaam aliliambia gazeti hili kuwa soko la nyumba kwa wateja wenye uwezo wa kawaida na wa chini limeyumba kwa kuwa uwezo wa watu kifedha umeshuka.
“Sasa hivi soko la nyumba limepungua, kodi ni miezi sita na mitatu zile kodi za mwaka sasa hivi zimekuwa ni historia, sasa hivi hakuna hela na wenye nyumba wanalazimika kushusha bei.
“Maeneo ya Kimara Baruti ipo nyumba moja ya kisasa kabisa ambayo mmiliki wake alikuwa akiipangisha kwa laki tano kwa mwezi, amekaa nayo muda mrefu mpaka sasa ameishusha laki tatu na nusu lakini bado hijapata mpangaji na pengine anaweza kushusha zaidi.
“Fremu ndiyo zimeshuka mara dufu, watu kila leo wanaachia frem kwa kuwa hakuna biashara, Yaani naweza kusema wengi wanaoweza kubaki ni wale wanaofanya biashara ya chakula kwa vile watu ni lazima wale, lakini biashara nyingine hizi ni mtihani kweli kweli,” anasema.
Jonas anasema. “Sasa hivi ukipita barabarani unaweza kuona watu wengi wakihama, siyo wanahamia kwenye nyumba zao, wengi wanatoka kwenye nyumba za gharama na kuhamia kwenye nyumba za gharama nafuu,” alisema.
Kuhusu viwanja anasema. “Miaka miwili nyuma kwa mfano ilikuwa haiwezi kupita miezi miwili sijauza kiwanja, lakini sasa hivi tangu mwezi wa kwanza hata mtu wa kuulizia tu sijampata, kwa kweli hali ni ngumu sana,” anasema.
Juma Hassan ambaye ni dalali wa nyumba na viwanja maeneo ya Tabata, anasema kuanzia kipindi cha mwaka 2016 kurudi nyuma, kwa mwezi alikuwa akipata wateja wa uhakika zaidi ya 20 ambao anawatafutia nyumba na kuzilipia.
“Na hawa siyo wale wa chumba kimoja, ni mtu anataka nyumba nzima labda ya Sh 500,000 kwa mwezi ama upande wa Sh 350,000,” anasema Hassan.
Anasema kwa upande wa viwanja, ilikuwa pia akipata eneo zuri kuna watu alikuwa anawajua kwamba akiwapigia simu, moja kwa moja wanaenda na kulipa kisha wanajenga nyumba za kupangisha (apartments).
“Kwa sasa hivi unamaliza mwezi ukijitahidi sana una wateja wawili, na kwenye hao wawili mnajikuta mko madalali mpaka wanne mnagombania, inabidi mgawane hela, viwanja ndiyo kabisa, mimi ninacho kimoja hapo karibu na Songas Kinyerezi, kinauzwa Sh milioni 30, ninamiezi mitano sasa sipati hata mtu wa kwenda kuangalia,” anasema.