Na Allan Vicent, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Burian amewataka viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo kusimamia maslahi ya wakulima katika vyama vyao ili mazao yanayozalishwa yawanufaishe.
Batilda amesema hayo hayo wakati akizungumza na viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa wakulima wa pamba na tumbaku mkoani humo.
Amesema kuwa kilimo kina manufaa makubwa sana kwa jamii kama kitasimamiwa ipasavyo na viongozi waliopewa dhamana, tatizo lililopo baadhi ya viongozi hawatimizi wajibu wao kwa kuzingatia maadili, taratibu na sheria za vyama hivyo.
Ametaja baadhi ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya wakulima kuwa ni vitendo vya wizi, ubadhirifu, utoroshaji mazao ya wakulima, matumizi mabaya ya madaraka na madeni sugu, hivyo akaagiza viongozi wapya kukomesha kero hizo.
“Mambo mengine ni madeni makubwa ya mabenki kwa wakulima na vyama vyao, udhaifu na kasoro za upandaji miti na malipo yake, ukosefu wa viwanda vya kuchakata mazao ya wakulima na makampuni ya wazawa kuchelewesha malipo.
‘Changamoto nyingi zinazowakabili wakulima, vyama vya msingi na vyama vikuu zinasababishwa na viongozi wasio waadilifu, ni matarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtabadilika, vinginevyo tutachukua hatua stahiki’, amesema.
Balozi Batilda amewataka kujiepusha na rushwa na kusimamia vizuri mikopo inayotolewa kwenye vyama vya msingi, kudhibiti kasoro kwenye mfumo wa upandaji miti na makato ya malipo na kusimamia ipasavyo zoezi la upandaji miti.
Ameagiza viongozi wa vyama vikuu vya ushirika Mkoani humo WETCU, MILAMBO na IGEMBENSABO kusimamia ipasavyo watendaji wa vyama vya wakulima ili watekeleze wajibu wao kwa kuzingatia taratibu na sheria na kutanguliza maslahi mkulima.
Amesisitiza kuwa serikali inathamini sana ushirika na itaendelea kuanzisha na kuvijengea vyama mazingira mazuri ya uzalishaji, ushindani na masoko kwa mujibu wa sheria ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake.
‘Ushirika ni nyenzo muhimu sana ya kujenga uchumi wa nchi, msituangushe shirikianeni ili kuleta tija kwenye uchumi wa kati ambao msingi wake mkubwa ni viwanda, kutoa ajira, kuinua pato la mkulima na kuchangia pato la taifa’, alisema.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani hapa Absalom Geofrey alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo, weledi na kuwawezesha kutoa mchango mkubwa katika vyama wanavyoviongoza.
Amesema mafunzo hayo yameratibitiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi vyama vya Ushirika (COASCO), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MUCCOBS), TAKUKURU na TRA.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Johnson Kimambo kutoka MUCCOBs alisema kupitia mafunzo hayo viongozi wapya wataelewa dhana, misingi na uendeshaji wa ushirika na kuitekeleza inavyotakiwa.