AMINA OMARI
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amesema atamshauri Rais Dk. John Magufuli kuona namna kuwapokonywa kiwanda cha chai Mponde, Mfuko wa Hifadhi ya PSSF kutokana na kushindwa kukiendeleza.
Hayo aliyasemwa wakati wa kikao cha baraza la madiwani la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa 2018/19 kwa Halimashauri ya Wilaya ya Bumbuli kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilaya humo.
Alisema Serikali ilitoa uwekezaji wa kiwanda hicho, lakini kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa na mfuko huo.
“Tulitegemea baada ya kiwanda kupata mwekezaji mpya, kitaanza uzalishaji, tayari wananchi na halimashauri walikuwa na matumaini makubwa ya kukufuka kiwanda hiki,”alisema.
Alisema kutokana na ukimya wa mfuko huo, ipo haja ya kumshauri rais kuvunja mkataba na kutafuta mwekezaji ambaye ataweza kuleta matumaini ya wananchi wa Bumbuli.
“Asilimia 80 ya mapato ya halimashauri yanategemea kiwanda hiki, kusimama kwa uzalishaji kumechangia kushuka mapato,”alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka watendaji kuhakikisha wanaimarisha makusanyo yamapato katika halimashauri hiyo ili iweze kujiendesha kwa kutekeleza miradi ya maendeleo, badala ya kuwa tegemezi.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, January Lugangika aliwataka wataalamu kuzingatia kanuni bora za usimamizi ili kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi.
“Kama watendaji watasimamia kwa ukaribu ukusanyaji wamapato, kiwango cha makusanyo kitaongeza na hakutakuwa na mianya ya ukwepaji wa ushuru,”alisema.
Madiwani waligomea kikao kujadili hoja za CAG kwa saa moja kutokana na kudai malimbikizo ya posho za vikao.Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya ufunguzi wa baraza hilo chini ya mwenyekiti wake, Shehiza aliomba baraza lijigeuze kama kamati ili kupata muafa wa hoja yao ya madai ya posho.