26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza amtaka CAG Nyamagana

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ngusa Samike, amuandikie barua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwenda mkoani humo kufanya ukaguzi wa kina kutokana na upotevu wa zaidi ya Sh Bilioni 3.15 zinazotolewa na serikali kwa makundi maalum katika Halmashauri ya Jiji hilo.

Mhandisi Gabriel ametoa maagizo hayo Mei 30, 2022 jijini humo kufutia taarifa aliyopewa na Kamati Maalum aliyoiunda mwezi mmoja uliopita kuchunguza ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wajasiriamali kutoka makundi maalum ya vijana wanawake na watu wenye ulemavu.

Alisema  kamati hiyo ilitembelea Kata 10 kati ya 18 zilizomo ndani ya halmashauri hiyo na vikundi 156 kati ya 337 ndipo ilipobaini Sh bilioni 1.9  ziliidhinishwa na kamati ya huduma na mikopo  kwa miaka mitatu mfululizo  ingawa kwa mujibu wa  mweka hazina wa halmashauri ya jiji la Mwanza zilizotolewa ni Sh bilioni 5.2.

“Hivyo kwa maelezo hayo kamati imebaini kwa miaka mitatu mfululizo  kiasi cha Sh bilioni 3.15 zilitolewa bila kufuata utaratibu, hizo ni kata 10 tu ambazo kamati imetembelea imebaini ubadhilifu mkubwa kiasi hiki, je ingetembelea kata zote 18 zenye vikundi 680 sijui upigaji ungefika kiasi gani,” amehoji na kuongeza:

“Haya yote yanatokea lakini tunaye Mkaguzi wa ndani kama jicho lake halioni kama kanuni, taratibu na sheria zinavunjwa kwenye  utoaji wa mikopo ya  asilimia 10 inabidi CAG aje atusaidie kufanya ukaguzi maalum na wa kina, ripoti yake itatusaidia kuchukua hatua sahihi,” amesema Mhandisi Gabriel.

Amefafanua kwamba wakati wakimsubiri CAG kwenda kufanya ukaguzi huo, taratibu zingine kwenye matumizi ya fedha zitaendelea kwa mujibu wa sheria huku akiomba sekretarieti kuwepo na mfumo wa kidigitali nchi nzima au kila mkoa wa kuripoti na kurekodi taarifa zote za utaratibu na mchakato  wa vikundi kutoka makundi maaalum vinavyokopeshwa fedha za asilimia 10.

Aidha, Mhandisi Gabriel ameruhusu mikopo hiyo kuanza kutolewa katika halmashauri zote mkoani humo baada ya kusitisha Aprili 25, mwaka huu ili elimu ya kanuni, sheria na taratibu za mikopo hiyo itolewe kwa waratibu na wakopaji lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi wa fedha na kutathmini utelelezaji wa kanuni hizo kutoka serikali za mitaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles