25.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 5, 2024

Contact us: [email protected]

RC Malima ahimiza wachimbaji madini kuhifadhi mazingira

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wachimbaji wa madini nchini wametakiwa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Hayo yamebainishwa Mei 4, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Madini Kitaifa inayofanyika mkoani humo kwa kuratibiwa na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania(FEMATA).

Malima amesema baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakitekeleza shughuli zao kwa kutokujali utunzaji wa mazingira hali iliyosababisha jamii kuwa na mtazamo kwamba kundi hilo si rafiki kwa mazingira kwa kuwa pia baadhi yao hutiririsha maji yenye kemikali yanayohatarisha afya za wanajamii.

“Naomba niweke msisitizo katika utunzaji wa mazingira, maana shuhuli za uchimbaji zimesababisha jamii kudhani kwamba wachimbaji ni watu wasiojali utunzaji wa mazingira, nakumbuka nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuna wachimbaji walikuwa wanatiririsha uchafu unaotokana na mabaki ya uchimbaji kutoka kwenye migodi yao kwenda kwenye makazi ya wananchi.

“Kama mnajua kwamba mtatumia ardhi iliyopo hapa nchini kwa shughuli za uchimbaji na baadaye mtaiacha ili na vizazi vijavyo vije viitumie lazima mtatunza na kuhifadhi mazingira ninauhakika kwamba baadhi yenu mnatunza mazingira lakini katika hali halisi samaki mmoja akioza kati ya 10 wote wameoza acheni kushiriki kwenye uharibifu wa mazingira,” amesisitiza Malima.

Aidha, amewasihi wachimbaji hao kushiriki katika kampeni ya upandaji miti kimkoa inayofanyika mkoani humo iliyolenga kupanda miti milioni 23.

“Ndani ya mkoa wetu wa Mwanza tumeanza kampeni ya kupanda miti milioni 23 nawaombeni na nyie FEMATA mshiriki katika zoezi hilo ili kwa pamoja tuijenge nchi yetu,” amesema Malima.

Katika hatua nyingine, Malima ameipongeza FEMATA kwa kupiga hatua katika uchimbaji ambapo sasa wanatumia teknolojia za kisasa ikilinganishwa na miaka 15 iliyopita walipokuwa wakichimba kwa kutumia vifaa duni ikiwemo sululu na kusema kwamba shirikisho hilo ni mfano wa kituambacho kinawezekana endapo mtu akidhamilia na kubainisha kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaongeza fursa hivyo wazitumie ili kuendelea kujiletea maendeleo na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Rais wa FEMATA, John Bina ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwawekea mazingira rafiki katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira, Bina amesema katika kuadhimisha wiki ya madini miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na
kutoa elimu kwa wanachama wao kuhusu utunzaji wa mazingira lengo likiwa ni kuwawezesha kutambua umuhimu wa mazingira safi na bora kwa maendeleo ya taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles