33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

RC MAKONDA USIRUDI NYUMA

Na Kulwa Karedia

“NIKO tayari kupoteza nafasi yangu ya mkuu wa mkoa, najua siku moja Mungu ataniuliza nilipokupa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Rais wako Magufuli, watoto waliangamia kwa dawa za kulevya, sitaki nifike mbinguni nisiwe na jibu.”

Hii ni kauli nzito na ya kwanza kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hadharani. Ilikuwa ni kauli ya kusisimua pale alipoamua ‘kujilipua’ kutaja askari polisi 9 siku ya kwanza na wasanii maarufu kuwa ni watuhumiwa au watumiaji wa dawa za kulevya. Siku ya pili akaongeza tena polisi watatu.

Niliposikia mwenyewe nililazimika kuacha kuendelea na majukumu yangu pale ofisini na kujiuliza, hivi huyu ni Makonda ninayemjua au leo ni ule msemo wa vijana wa siku hizi ‘amepotea njia’. Nikakuta ni yeye halisi.

Nikavuta pumzi kidogo, nikainuka kwenye kiti change, nikaendelea kumsikiliza vizuri hasa pale alipoanza ‘first eleven’ yake watu wanaodaiwa kusaidia biashara ya unga na watumiaji.

Nilishtushwa na Makonda pale alipotaja vijana wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ,kwamba wapo  tisa wanaosaidia  mtandao wa dawa za kulevya.

Hapo niliona wazi upele umepata mkunaji kwa kweli. Miaka nenda rudi tumekuwa na viongozi wengi wa kitaifa ambao wameishia kusema wana majina lakini hawawataji. Nakumbuka Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni mmoja wapo, kwa vile walisema tumuache mzee apumzike, leo si siku yake kumjadili hapa.

Leo naanza kwa kukupongeza Makonda kwa ushujaa wako ambao umetukuka katika hili, ni ukweli usiopingika kwamba hivi sasa nguvu kazi ya taifa imezidi kupuputika kila kukicha na watu waliopewa dhamana ya kusimamia mambo haya wapo, vijana ambao wana nguvu zao wamegeuka kuwa mateja utafikiri dola haipo.

Ndugu yangu Makonda, naamini ulisoma vizuri gazeti la MTANZANIA mwezi uliopita namna lilivyoweka picha za wasanii ambao ukiwaangalia afya zao, utafikiri walikuwa wanaishi jangwani ambako hakukuwa na mahitaji yoyote muhimu kwa  binadamu. Kijana kama Chidi Benz huwezi kumsimamisha dakika 10 kutokana na mwili kupoteza uhalisia wake. Je viongozi wanafurahi hii hali?

Makonda najua vita ulivyovianzisha ni vikali kwa sababu vina mtandao, lakini nakuhakikishia  hautashindwa kwa sababu vina lengo zuri la kukomboa kizazi hiki, simamia msimamo wako ili ukifika kwa Mungu siku moja uwe na majibu mazuri.

Umeonesha tofauti ya watangulizi wako na mawaziri wengi ambao walikuwa wanapewa dhamana ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, siku zote wanapoteuliwa huja na maneno matamu. Wa mwisho kuja na maneno hayo ni Mwigulu Nchemba ambaye ana jina kubwa na maarufu, lakini utendaji katika hili umeporomoka kwa kasi ya aina yake, sijui kwa kweli amejifunza nini kutoka kwako.

Makonda, nakuhakikishia vita hii unaungwa mkono kwa asilimia mia moja na Watanzania wengi, kwa sababu hakuna mzazi ambaye anataka kuona mtoto wake anakuwa teja.

Hivi ni kweli kwamba polisi wetu wanavyoshinda doria za usiku na mchana huwa hawajui vijiwe na maeneo ambayo dawa hizi zinapatikana?

Makonda umewavua nguo, IGP Mangu, Kamishina wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Waziri Mwigulu ambao wamebeba dhamana kubwa ya mkoa wako. Pia umepeleka salamu zako bila kujua Idara ya Uhamiaji ambacho iko chini ya Mwigulu kuwa inawezekana kwenye mipaka na viwanja vya ndege nao wajitafakari katika hili.

Naamini umewafanya wajione wapo wapo tu na si kuwatumikia wananchi wao. Wamebaki kuwa wazee wa matamko pindi yanapotokea matukio na si utendaji.

Leo namalizia kwa kuwaomba Watanzania wenzangu, wakuunge mkono kwa kila hatua ili kukomesha tatizo hilo. Dar es Salaam bila dawa za kulevya au mateja inawezekana kabisa. Kwa lugha ya kwenu kule usukamani mnasema ‘wabhejaa’ pambana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles