26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

RC amwagiza DC kuunda kamati kuchunguza ujenzi Ihungo sekondari

Na Nyemo Malecela, Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali kuunda kamati itakayofanya kazi ndani ya siku saba kuchunguza ujenzi wa nyumba za walimu na bweni katika shule ya wavulana ya Ihungo iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani humo.


Mbuge alitoa maagizo hayo baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa nyumba za walimu wa shule hiyo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na serikali katika Wilaya ya Bukoba akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi ya Mkoa na Wilaya hiyo pamoja na wakuu wa idara zote.


“Mkuu wa Wilaya nakuagiza uunde kamati itakayofanya kazi ndani ya siku saba kuchunguza miradi yote inayojengwa na TBA na makampuni mengine katika shule hii na mkandarasi atoe ushirikiano, ndani ya siku 14 kila kitu kiwe kimekamilika.


“Haiwezekani madirisha hayana nyavu, madirisha yamechakaa mapema kabla ya walimu kuanza kuyatumia wakati uwekeji wa mifumo ya umeme katika nyumba hizo haukidhi viwango vya thamani za nyumba zenyewe,”amesema.


Pia Mbuge ameagiza mkandarasi wa TBA kuhakikisha ujenzi wa mfumo wa maji taka na maji safi katika bweni la shule hiyo pamoja na mfumo wa jiko la Bio_gas vinakamilika kwa ufasaha.


Katika ziara hiyo, Mbuge na viongozi alioambatana nao walitembelea mradi wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto inayojengwa katika zahanati ya Buhembe, mradi wa maji wa Burugo, ujenzi wa chuo cha Veta unaotekelezwa katika kata ya Burugo na kukamilisha ziara hiyo kwa kuongea na madiwani wote wa kata za Jimbo la Bukoba Mjini.


Katika mradi wa ujenzi wa wodi ya mama mjamzito na mtoto ya zahanati ya Buhembe, Mbuge alimuagiza Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Yeba Clavery kuhakikisha anasimamia fedha ambazo ni zaidi ya milioni 334 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo zinatosheleza.


Naye Kaimu Mhandisi, Method Rwelamira amesema ujenzi wa wodi hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2019 imefikia asilimia 96.


“Tunatarajia kukamilisha ujenzi Agosti 30 mwaka huu kwa kuwa vifaa vyote vya kukamilisha ujenzi huu vipo,” amesema.


Katika mazungumzo kati ya Mbuge na madiwani, aliwataka madiwani kudumisha mshikamano na kuachana na mipasuko na majungu ili kwa pamoja waweze kusimamia miradi inayotekelezwa katika kata zao.


Pia madiwani hao wametakiwa kusimamia ukusanyaji wa kodi, mradi wa TASAF pamoja na kuwaelimisha wananchi ili kupunguza changamoto zinazojitokeza na walengwa wapate haki wanayostahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles