27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

RASILIMALI ZETU ZITUMIKE KUKUZA UCHUMI BADALA YA FEDHA TASLIMU

rasilimali

NA YERICKO NYERERE,

 KATIKA kujenga taifa ni lazima tuwe na kipaumbele, na katika taifa lililoparaganyika kama Tanzania linahitaji mbinu tofauti sana katika kufikia malengo ya taifa la uchumi imara.

Hapo awali tulishauri Serikali hii iwe na vipaumbele muhimu katika kujenga taifa, hili lilitokana na ukweli kwamba, taifa na Serikali ya Rais John Magufuli haikuwa na dira wala kipaumbele kilichoonekana kwa umma, kila jambo tuliligusa kana kwamba hatuna malengo.

Juzi nimesikia na kumuona Rais Magufuli anasema Tanzania inapanga kununua ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262, ambayo inatarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018.

Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kuwasili Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.

Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika. Hii ina maana kwamba, taifa litakuwa na ndege 6. Safi sana. Nimefuatilia kwa mwezi sasa tangu shirika la ndege kupitia pangaboi zake lianze kazi, nikiri kuna mabadiliko makubwa ya kimfumo, nimeona wanatumia mfumo ambao unatumiwa na Emirates na Rwanda.

Ni mfumo mzuri katika dunia mpya ya biashara ya anga… Pia udhibiti wa watumishi wa umma katika kusafiri kumeongeza faida kubwa kwa shirika hili, ifahamike kuwa mteja mkubwa wa biashara ya anga nchini Tanzania ni Serikali kupitia watumishi wake. Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka jana TASAF pekee ndiyo iliyovunja rekodi kwa kulipa nauli ya ndege yenye thamani ya Sh bilioni 3.

Utaratibu mpya wa serikali hivi sasa watumishi wote wanaosafiri nchini watatumia ATCL, na malipo ya nauli zao yanalipwa kupitia bajeti ya wizara husika, yaani mfano Wizara ya Nishati na Madini katika bajeti yao wameainisha kwamba watatumia Sh bilioni 59 katika safari za ndani, basi upembuzi yakinifu unafanywa kujua safari zote zitakazotumia ndege, hivyo fedha inapelekwa kabisa ATCL.

Kinachofuata katika wizara muda wa watumishi wao kusafiri ukifika wanapeleka majina mapema wakahakikiwe na wakatiwe tiketi.

Kiongozi wa Ethiopia alipoamua kujenge Shirika la Ndege la Ethiopia aliamua kwa dhati kusimamisha baadhi ya mambo katika taifa kwa mwaka mzima ili ajenge shirika hilo bora barani Afrika, moja ya mambo yaliyosimamishwa ni elimu na afya, yaani wizara hizo hazikupewa fedha ya bajeti kwa mwaka huo, badala yake fedha ikanunulia ndege… Nchini kwetu tuombe kiongozi yeyote asije kuiga staili hii, kwani Ethiopia walikufa watu wengi kwa kukosa huduma za afya.

Msimamo wangu toka awali ni kwamba, ili taifa liendelee ni lazima tuwe na vipaumbele na kila kipaumbele tuhakikishe kinafika mwisho katika utekelezwaji, na hili bado naendelea kusimamia na kuamini kwamba hii ndiyo njia maridhawa ya kuongoza nchi duniani kote.

Tanzania ina vitu vitatu ambavyo vikipangwa kwenye vipaumbele vya taifa kimoja baada ya kingine, taifa litapona na kuwa la mfano barani Afrika. Mosi; nishati na madini. Pili; bandari/maji, tatu; anga.

Kati ya hivi, naamini taifa likiamua kutekeleza kimoja kimoja mpaka mwisho litafanikiwa na kuwa taifa la mfano barani Afrika.

Mwaka juzi nilifika katika miji ya Berlin na Bremen nchini Ujerumani, nikapata fursa ya kuzuru sehemu ya uhifadhi wa kumbukumbu za makoloni ya Ujerumani, moja ya makoloni hayo ni Tanganyika.

Katika kumbukumbu zile ipo michoro ya madini ya Tanganyika ambayo inaonyesha kuna aina 360 za madini katika ardhi ya Tanganyika, ikiwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na aina nyingi za madini.

Mtazamo wangu, Rais Magufuli hahitaji kutumia amana ya fedha ya nchi taslimu katika kutekeleza vipaumbele vyake vya taifa, bali atumie rasilimali hizi katika kulijenga taifa, dunia imebadilika, ipo katika uhitaji, wewe unayo gesi, yule anao utaalamu, wewe unayo uranium, yule anavyo vinu vya nyuklia, wewe unayo Tanzanite, yule ana kiwanda cha vito, wewe unacho chuma, yule ana kiwanda cha chuma anahitaji chuma.

Katika mazingira kama haya, unatoaje fedha taslimu kununua ndege ikiwa wenye kiwanda cha ndege wanahitaji madini ya zinki na wanaagiza China ilhali China wanayapata Tanzania madini hayo?

Kwanini usimwambie Boing alete ndege 40 kisha aje achukue madini hayo Tanzania kwa miaka10. Unatoaje fedha taslimu kujenga reli ilhali Wachina hawa wanahitaji madini ya safaya?

Kwanini usimwambie Mchina ajenge reli kisha avune madini ya safaya kwa miaka 10. Unatoaje fedha kununua ndege za kivita ilhali Warusi wanahitaji uranium kwa ajili ya viwanda vyao vya kurutubishia silaha za kikemia?

Kwanini usimwambie Mrusi aje avune madini ya uranium kwa miaka 10? Kwanini hatujifunzi kutoka kwa nchi zilizofanikiwa, mfano Singapore, Malaysia, China nk?

Nchi zenye rasilimali nyingi kama Tanzania haiwezi kutumia mfumo wa nchi zisizo na rasilimali kama Kenya na Rwanda katika kufikia uchumi wa kisasa.

Lazima tutumie rasilimali zetu kujenga taifa, lakini tukumbuke njia ya kuzitumia rasilimali hizi si lazima ziwe zile zinazopendekezwa na wazungu.

Tuamue sasa, mfano  Zambia, Uganda na nchi nyingine zikihitaji gesi tutumie wazungumzaji wazuri, Kenya wakihitaji gesi tunapima kiasi cha gesi wanayoihitaji kisha kinathaminishwa na kuwapa kazi ya kujenga mji wa Dodoma wenye thamani ya Sh trilioni 12.

Zambia wakihitaji vilevile tunawapa kazi ya kusambaza maji nchi nzima kulingana na mahitaji yao. China vile vile wakihitaji makaa ya mawe, tunawaambia kwamba tunahitaji reli ya kisasa kutoka Tanzania hadi Rwanda, hakuna kutumia fedha ya umma kufanya jambo ambalo lingefanywa na rasilimali tulizonazo …urais hauna chuo.

Dubai, China, Malaysia, Korea Kusini na Kaskazini, Singapore walifanikiwa kutumia mfumo huu, hivyo tuna kila sababu ya kuchagua nani tushirikiane naye kwa masilahi ya Taifa.

Pamoja na kwamba kuna masharti na mikataba ya kimataifa inayoweza kutuzuia kufanya biashara ya namna hii, lakini lazima tujifunze kwa waliofanikiwa kupitia njia hii.

Katika hili la kuchagua kipaumbele kuwa sekta ya anga, nakupongeza sana, mengine yaache yajiendee kama yalivyo, lakini tekeleza moja kwa vitendo na lifike mwisho kabisa, hakika matokeo chanya yatapatikana, ijapokuwa unaathiriwa na siasa za vyama.

 KWA MAONI – 0715865544 au 0755865544

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles