TURIN, ITALIA
KIUNGO wa timu ya Juventus, Aaron Ramsey, amethibitisha kumuomba radhi mshambuliaji wa timu hiyo Cristiano Ronaldo baada ya kuiba bao lake kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Lokomotiv Moscow.
Katika mchezo huo, Juventus walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tatu lililofungwa na Ramsey baada ya shuti kali lililopigwa na Ronaldo, wakati mpira huo unaingia nyavuni ukiwa kwenye mstali Ramsey aliamua kumalizia wakati hakuwa na sababu yoyote ya kuupiga mpira huo, hivyo bao hilo likawa lake badala ya Ronaldo.
Kitendo hicho kilimuumiza Ronaldo na hakuweza kushangilia, hivyo hadi dakika 90 zinamalizika Ronaldo hakuweza kuwa na bao, alikwenda moja kwa moja kwa kocha wake Maurizio Sarri na kumlalamikia kitendo hicho kilichofanywa na Ramsey.
Bao hilo lingemuingiza Ronaldo kwenye rekodi mpya ya kuzifunga jumla ya timu 34 tofauti kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika historia yake, ila Ramsey akakatisha mipango hiyo.
Hivyo Ronaldo anabaki kuwa amezifunga jumla ya timu 33, sawa na mpinzani wake Lionel Messi na Raul, lakini Ramsey amethibitisha kumuomba radhi Ronaldo kwa kitendo hicho.
“Kabla sijamalizia mpira kuuweka langoni nilidhani kuwa mlinda mlango yupo karibu sana kuweza kuuokoa mpira huo, hivyo nikaona bora nihakikishe unazama moja kwa moja kwa kuumalizia.
“Niweke wazi kuwa, nimemuomba radhi Ronaldo na ninaamini amepokea ombi langu, najua alikuwa na lengo la kutaka kuweka rekodi, ila ninaamini ataendelea kufanya makubwa,” alisema mchezaji huyo.
Ushindi huo umewafanya Juventus kuwa vinara kwenye msimamo wa kundi lao D na kujihakikishia kuingia hatua ya 16 bora wakiwa na pointi 10 baada ya kucheza michezo minne.