ALIYEKUWA nyota wa klabu ya Chelsea, Ramires, ameanza kufanya vizuri katika klabu yake mpya ya Jiangsu Suning ya nchini China kwa kuipa bao juzi dhidi ya Anzhi Makhachkala.
Mchezo huo ulikuwa wa kirafiki, huku Ramires ukiwa ni wa kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili Januari, mwaka huu kwa kitita cha pauni milioni 25 kutoka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England.
Kiungo huyo wa timu ya Taifa ya Brazil aliitumikia klabu ya Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano na nusu kabla ya kujiunga na klabu hiyo ya nchini China.
“Nimefurahi na mapokezi ya nchini China na nimeanza vizuri kwa kufunga bao katika mchezo wangu wa kwanza, japokuwa ni mchezo wa kirafiki, lakini nitakuwa nimeandika historia.
“Ninahitaji kuzoea mazingira, lakini haitakuwa ngumu sana, nitakwenda sawa na kufurahia Ligi ya huku China,” alisema Ramires.
Hata hivyo, klabu hiyo ipo mbioni kuinasa saini ya mchezaji wa Shakhtar Donetsk ambaye ni raia wa nchini Brazil, Alex Teixeira, kwa kitita cha pauni milioni 35.