ANKARA, UTURUKI BARUA aliyoiandika Rais wa Marekani, Donald Trump kwenda kwa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan akimshauri asiwe “mpumbavu” imetupwa kwenye debe la taka.
Rais huyo wa Uturuki, Erdogan aliitupa barua hiyo iliyoandikwa Oktoba 9 mwaka huu na kutumwa baada ya vikosi vya Marekani kuondolewa Syria.
Rais Trump alimwambia Erdogan: “Usijifanye kuwa na nguvu. Usiwe mpumbavu!”
Vyanzo vya ofisi ya rais wa Uturuki vimeiambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kuwa barua hiyo “ilimkasirisha sana” Rais Erdogan.
Siku ambayo barua hiyo ilipokewa, Uturuki ilianza operesheni yake dhidi ya vikosi vya Kikurdi katika eneo la mpakani.
“Wacha tufikie mpango mzuri! Bilashaka hutaki kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu, na mimi pia sitaki kuhusika na uharibifu wa uchumi wa Uturuki – na nitafanya hivyo,” Trump alisema katika barua hiyo.
“Historia itakuhukumu kwa haki ukishughulikia suala hili kwa njia ya kibinadamu. Itakuhukumu daima kama shetani kwa maovu”.
Katika majibu yake, vyanzo katika ofisi ya rais wa Uturuki vilisema: “Rais Erdogan alipokea barua, na kupinga vikali yaliyomo na kuitupa kwenye pipa la taka.”
Rais Trump alimwambia Erdogan: ‘Wacha tufikie mpango mzuri!’
Rais Trump amelaumiwa vikali kwa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria huku wakosoaji wakisema kuwa hatua hiyo iliipatia Uturuki nafasi ya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi nchini humo.
Ukosoaji mkubwa umetoka ndani ya chama chake cha Republican.
Katika hatua isiokuwa ya kawaida, wabunge 129 wa chama cha Republican katika bunge la uwakilishi waliungana na wenzao wa chama cha Democratic kupiga kura ya kupinga uamuzi huo siku ya Jumatano.
Azimio hilo la pamoja ambalo pia lilimtaka rais Erdogan kukomesha mara moja oparesheni ya kijeshi dhidi ya vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi, lilipitishwa kwa kura 354 – 60.
Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi pia alikutana na Rais Trump, kujadili suala hilo katika mkutano uliokumbwa na majibizano makali yaliyochangia yeye na kiongozi wa wachache katika bunge la Seneti, Charles Schumer, kuondoka katika chumba cha mkutano huo.
Viongozi wa Republican walikosoa vikali hatua hiyo ya Pelosi wakisema ni ukosefu wa “nidhamu”, na kumkosoa kwa “kuondoka katika mkutano huo”.
Pelosi na Trump pia walilaumiana kwa kile “kilichotokea”, na baadae Trump akaweka kwenye Twitter picha ya majibizano kati yao.
Lakini picha hiyo imesifiwa na Wanachama wa Democrats, ambao walisema ni ya “kishujaa” na ilimuonesha Pelosi akiwa “katika ubora wake”.
Pelosi pia aliifanya picha hiyo kuwa picha yake kuu katika mtandao wa Twitter.
Mapema siku ya Jumatano Rais Trump, alisema Marekani haitaingilia kati oparesheni ya kijeshi ya Uturuki nchini Syria, kwasababu nchi hiyo “sio mpaka wake”, na kuongeza kuwa Wakurdi ambao walikuwa washirika wao wa zamani “sio malaika”.
Wakati huo huo,
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amelihutubia bunge la Ujerumani kabla ya kuelekea mjini Brussels kuhudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, huku akibainisha kuwa nchi yake haitopeleka silaha Uturuki.