TEHRAN, IRAN
RAIS wa Iran, Hassan Rouhani amesema hatua za karantini zilizolenga kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona huenda zikachochea kufanyika maandamano kutokana na matatizo ya kiuchumi.
Katika mkutano wa baraza la mawaziri kuhusu janga la virusi vya corona, Rouhani alisema, njia rahisi ya kukabiliana na virusi hivyo ni kuzifunga shughuli zote.
Maambukizi ya virusi vya corona pamoja na idadi ya vifo vilipungua kwa kiasi kikubwa mnamo mwezi Mei baada ya hatua kubwa za karantini kuchukuliwa nchini humo. Lakini tangu wakati huo, idadi hiyo imeongezeka tena na maofisa wa serikali wanasema kuwa kufunguliwa kwa shughuli nyingi kumesababisha ongezeko hilo.
Maafisa wa Iran wamekuwa na hamu ya kuondoa vizuizi kwa uchumi wake ambao tayari umedhoofishwa na vikwazo vya Marekani vilivyowekwa mwaka 2018 baada ya serikali ya Trump kujiondoa katika mkataba wa nyuklia wa uliofikiwa mwaka 2015.