BANJUL, GAMBIA
MAJESHI kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) yakiongozwa na Senegal, yamepiga kambi katika mpaka na Gambia, yakijiandaa kumng’oa madarakani Rais Yahya Jammeh (51) iwapo ataendelea kung’ang’ania madaraka.
Ecowas imekuwa ikitishia kumwekea Jammeh vikwazo au kuingilia kijeshi nchini mwake iwapo hataondoka madarakani hadi saa ya mwisho ya kumalizika kwa muda wake ambayo ilikuwa usiku wa manane wa kuamkia jana.
Wakati majeshi hayo yakipiga kambi eneo hilo tayari kwa lolote kwa baraka ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), Mkuu wa Majeshi wa Gambia, Jenerali Ousman Badjie ametangaza kutoliingiza jeshi lake vitani iwapo majeshi ya kigeni yataingia katika ardhi ya taifa hilo.
Jenerali Badjie alitoa kauli hiyo muda mfupi tangu Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz, kuondoka Gambia baada ya kushindikana kwa jitihada za mwisho za kumshawishi Jammeh aachie ngazi kwa hiari.
Jenerali Badjie, awali wakati Rais mteule wa Senegal, Adama Barrow alipotangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Desemba mwaka jana, alimuahidi mgombea huyo wa upinzani ushirikiano baada ya Jammeh pia kukubali kushindwa.
Lakini alibadili msimamo baada ya Jammeh aliye madarakani kwa miaka 22 kugeuka kwa kuyakataa matokeo yaliyompa ushindi Barrow.
Jenerali Badjie ambaye kauli yake ya kutangaza kuwa nyuma ya Jammeh ilizua hofu ya umwagikaji wa damu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “hatuwezi kujihusisha kijeshi kwa sababu huo ni mgogoro wa kisiasa”.
Ofisa huyo wa ngazi ya juu katika Jeshi la Gambia, aliongeza kwa kusema kuwa hawezi kuwaingiza vijana wake katika mapigano ya kipuuzi.
“Nawapenda watu wetu na kama wanajeshi wa kigeni wakiongozwa na Senegal wakiingia nchini kwetu, tutasalia kama tulivyo,” alisema kiongozi huyo wa kijeshi huku akionyesha mikono juu kama ishara ya kusalimu amri.
Muda wa Rais Jammeh umefikia kikomo usiku wa manane wa kuamkia jana, lakini bado amekaidi kuachia ofisi baada ya kushindwa na mpinzani wake.
Ung’ang’anizi wake umezusha mashinikizo ya kumtaka aachie ngazi kutoka kwa mataifa ya Afrika Magharibi, baada ya wiki kadhaa za kushindwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia.
SABABU YA SENEGAL KUONGOZA KAMPENI
Nigeria na Ghana mbali ya kuandaa meli za kivita tayari kwa lolote, zimepeleka majeshi, ndege za kivita Senegal na sasa askari wakiwa na silaha wamekusanyika katika mpaka wa Gambia.
Ecowas iliipa Senegal jukumu la uongozi kwa sababu taifa hilo limeizunguka Gambia pande zote, isipokuwa baharini.
Aidha, mataifa hayo yaliwahi kuungana chini ya Shirikisho la Sene-Gambia lililoundwa Februari mosi mwaka 1982 kufuatia makubaliano baina yao yaliyosainiwa Desemba 1981.
Hata hivyo, Senegal ililivunja shirikisho hilo Septemba 30, 1989 baada ya Gambia kukataa kuelekea muungano kamili wa mataifa hayo.
Taarifa zinasema kuwa katika operesheni hiyo, Mkuu wa Majeshi wa Senegal, Jenerali Francis Njie, ndiye atakayeongoza mapambano hayo yanayohusisha wanajeshi 860 kutoka Nigeria na 500 kutoka Senegal.
Pia, watakuwapo makomandoo maalumu 60 watakaokuwa na jukumu la kumsaka na kumkamata Rais Jammeh akiwa hai au vinginevyo.
JESHI LA ECOWAS LASUBIRI IDHINI
Kanali Abdou Ndiaye, msemaji wa Jeshi la Senegal, alisema mambo yote yako tayari na wanajeshi wa Ecowas wako tayari kuingilia kati baada ya saa sita (usiku wa kuamkia jana) iwapo hawatapata suluhu ya kidiplomasia kwa mzozo huu wa Gambia.
Lakini pia wanajeshi hao wa Ecowas wanasubiri Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio la kutumiwa kwa hatua zozote zile kusaidia kuondolewa madarakani kwa Jammeh katika njia za amani.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, wanajeshi wote wa Gambia ni takriban 2,500 na hiyo inafanya ugumu wa kuwakabili na kuwashinda wanajeshi wa kanda hiyo.
Mashuhuda wanasema hali ya utulivu imetawala usiku wa kuamkia jana katika mji mkuu wa Banjul, ingawa majeshi yametawanywa pia katika mitaa ya mji huo.
BARROW AAPISHWA SENEGAL
Baada ya kuondoka Gambia, Rais wa Mauritania, Abdel Aziz, alisema kuna matumaini ya kufikia suluhisho la amani la kisiasa.
Rais huyo aliyasema hayo wakati akiwasili mjini Dakar, Senegal ambako amekutana na Rais wa nchi hiyo, Mack Sally na Barrow aliyetarajia kuapishwa baadaye jana katika Ubalozi wa Gambia nchini humo alikopatiwa hifadhi.
Kwa mujibu wa mkuu wa kamati ya maandalizi ya kuapishwa kwa Barrow, James Gomez, awali hafla ilikuwa ifanyike katika uwanja mkuu mjini Banjul.
Kutokana na uwepo wa hali ya kutoelewana, sasa uapishwaji huo utafanyika ubalozi wa Gambia, saa 10 jioni (saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki).
Barrow alitangaza kupitia mtandao wa Twitter, akiwaalika wananchi kuhudhuria.
Kabla ya muda wake kumalizika, Jammeh alitangaza hali ya hatari, iliyofuatiwa na taarifa ya juzi kuwa Bunge limemruhusu kubakia madarakani kwa miezi mitatu.
SERIKALI YAMSUSA JAMMEH
Kutokana na hali hiyo, Makamu wake wa Rais, Isatou Njie-Saidy, amejiuzulu sambamba na mawaziri kadhaa.
Pia mkuu wa Jeshi la Polisi ameacha utiifu, kwa kuamua kujitenga na Rais Jammeh.
Maofisa wengine wakiwamo wa Tume ya Uchaguzi, majaji na mawaziri, wameikimbia nchi kwa hofu ya usalama wao sambamba na raia 30,000.
Hayo yanajiri huku maelfu ya watalii kutoka Uingereza na Uholanzi, wakiendelea kuondolewa kutoka taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa ndege maalumu za kukodishwa.
Gambia ni maarufu sana kwa watalii kutoka Ulaya kutokana na fukwe zake, hasa wakati wa majira ya baridi.
Napenda habar zenu,muhimu ni kuendelea kubolesha