NEW YORK, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amesema kwamba, huenda akakutana na Kiongozi wa Urusi, Vladimir Putin, wakati wa ziara zake zitakazofanyika hivi karibuni katika eneo la Asia na Pacific.
Akizungumza jana katika mahojiano maalumu na jarida la FOX, Trump alisema kwamba, suala la kukutana na Rais Putin ni muhimu, kwa kile alichodai kwamba wanaweza kushirikiana kutafuta suluhisho kuhusu mgogoro Syria na Korea Kaskazini.
“Mbali na hayo, tukikutana tunaweza pia kuzungumzia jinsi hali ilivyo nchini Ukraine. Putin ni mtu muhimu sana kwa sababu anaweza kutusaidia kuhusu ugomvi wetu na Korea Kaskazini,” alisema Trump.
Rais Trump anatarajia kuanza ziara ya siku tisa kesho katika nchi za Japan, Korea Kusini, China, Vietnam na Ufilipino, ambayo itakuwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi katika Bara la Asia, kabla ya Novemba 10 kuhudhuria mkutano wa nchi wanachama wa nchi za Ushirikiano wa Kiuchumi Asia na Pasific (APEC), utakaofanyika nchini Vietnam na mwingine wa Umoja wa nchi za Kusini mwa Asia (ASEAN) utakaofanyika mjini Manila, Ufilipino.