RAIS wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ameanza ziara ya siku nne Ethiopia, akimwaguia sifa Waziri Mkuu, Abiy Ahmed Ali.
“Nimefika katika nchi iliyobadilika, nchi inayochipuka. Nchi inayofanyiwa mageuzi. Kwa niaba ya wote niliofuatana nao, naamini naweza kusema tuna fahari na kusifu moyo wenu wa ujasiri wa kuanzisha mageuzi kama haya,” Steinmeir alisema.
Mbali ya kukutana na Abiy, Rais huyo wa Shirikisho la Ujerumani alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde.
Abiy (42) ameanzisha mageuzi makubwa nchini hapa tangu April 2018, akiwaachia huru maelfu ya wafungwa wa siasa na kuanzisha mfumo wa uliberali wa uchumi.
Abiy pia amefikia makubaliano ya amani na nchi jirani ya Eritrea wanakotokea wakimbizi wengi wanaoingia Ujerumani.
Amefanikiwa pia kuweka uwiano wa jinsia katika nyadhifa za serikali.
Hata hivyo, bado mvutano wa ukabila unatishia umoja na mshikamano wa nchi hiyo, ambayo ina kiwango cha juu cha umasikini na ukosefu wa ajira.
Kutokana na changamoto hizo, Rais Steinmeier alitoa ahadi kuwa nchi yake itasaidia kwa uwezo wake wote kuleta ustawi na mageuzi zaidi Ethiopia.
“Nuru ya mapambazuko ya demokrasi inaweza kunawiri mpaka nje ya Ethiopia hadi barani Ulaya na kwa namna hiyo kuibadilisha pia picha ya Afrika barani Ulaya, picha inayoliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la mizozo na mvutano,” alisema.