24 C
Dar es Salaam
Saturday, July 6, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia: Matusi mitandaoni hayatanizuia kufanya mageuzi ya kiuchumi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema anafahamu kuhusu matusi yanayoendelea katika mitandao ya kijamii, lakini ameamua kukaa kimya kwani lengo lake kuu ni kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini.

Rais Samia alibainisha hayo Juni 11, 2024, wakati wa hafla ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka mashirika ya umma na binafsi iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilikuwa na kauli mbiu: “Mageuzi ya Mashirika ya Umma na Wajibu wa Kuchangia Maendeleo ya Tanzania.”

“Najua kuna matusi mengi ninayotukanwa, lakini najigeuza kuwa kama chura kiziwi ambaye hayasikii. Lengo langu ni kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi yetu ili maendeleo yapatikane,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alieleza hadithi ya chura aliyeshinda shindano kwa kupanda juu licha ya kelele nyingi za kujaribu kumvunja moyo. Chura huyo hakuweza kusikia kelele hizo na aliendelea mpaka akafanikiwa. Alijifananisha na chura huyo kwa kusema, “Mimi kazi mliyonipa nasimama na kuifanya. Matusi ninayotukanwa, na kelele ninazopigiwa, hazitanizuia kutimiza malengo yangu.”

Aliongeza kuwa, “Yeyote anayetaka kunikera, anikanyagie uchumi wangu. Katika mageuzi haya, tutakanyaga wengi ambao hawataki kwenda mbele na ndio watakaopiga kelele nyingi sana. Mliopo kwenye mashirika ambao hamtaki kukanyagiwa, nendeni mkafanye kazi ili kuleta maendeleo,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia kuhusu bandari, Rais Samia aliipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 153.9 kwa serikali. Alisema wale wanaopinga mageuzi hayo hawajui faida zake, na anaamini TPA itaendelea kutoa gawio kubwa zaidi kwa serikali kutokana na mageuzi yaliyofanyika.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema serikali inakamilisha mchakato wa kuandikisha mashirika ya umma kwenye soko la hisa ili wananchi wanunue hisa na kuwa wamiliki wa mashirika hayo. Pia, alieleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kufuta au kuunganisha mashirika yasiyofanya vizuri.

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alitoa taarifa ya kupokea gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi. Alisema hadi sasa wametoa gawio la shilingi bilioni 637, na wanatarajia kufikia shilingi bilioni 850 kufikia mwisho wa mwaka huu. Pia, alisisitiza umuhimu wa ubunifu na kuongeza mapato ya taasisi ili kuchangia mfuko mkuu wa serikali na kusaidia maendeleo ya taifa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, alisema bodi za mashirika ya umma zina wajibu wa kulinda maslahi ya umma kwa kusimamia utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa mashirika ya umma na taasisi kuendelea kuchangia uchumi wa taifa na kupunguza mzigo kwa serikali. Rais Samia alisisitiza kuwa mageuzi haya ni kwa manufaa ya wote, na wale wanaopinga hawataweza kuzima azma yake ya kuleta maendeleo nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles