Na Ramadhan Hassan, Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan atahitimisha wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), yatakayopambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo gwaride la vijana wa JKT.
Shughuli nyingine zitakazofanyika katika kilele kutakachofikiwa kesho kutwa (Jumatatu) ni maonyesho ya vifaa na burudani za ngoma za JkT na wasabi mbalimbali.
Akizungumza leo Jumamosi Julai 8, 2023 Waziri wa Ulinzi na JKT, Innocent Bashungwa amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika katika uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma.
“Nawakaribisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatatu kuanzia saa 12.30 asubuhi katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma. Karibuni ndugu wananchi kumsikiliza Rais na Amorim Jeshi Mkuu,”amesema.
Kilele cha maadhimisho hayo kimetanguliwa mbio za JKT Marathon, maonyesho ya bidhaa, huduma za jamii ikiwemo kutembelea na kufanya usafi katika Kituo cha Afya cha Chamwino jijini Dodoma.
Pia kutembelea Makao ya Taifa ya Watoto Chamwino na kugawa zawadi za vyakula na shughuli ya uchangiaji damu kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa.