Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi kuwa na utamaduni wa kutunza kumbukumbu zao kwa ajili ya maslahi yao, Taifa na kizazi cha baadae huku pia akitaka kuanzishwa kwa Tovuti ya Serikali itakayoweka kumukumbu za viongozi.
Dk. Samia ameyasema hayo leo Septemba 30, wakati akizindua tovuti ya kuhifadhi nyaraka za Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam uliohudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini na Taasisi.
Amesema familia ya Dk. Salim ndio waliokuja na wazo hilo la kuweka tovuti maalumu hivyo ni wakati sasa wa Serikali kufikiria namna ya kuanzisha tovuti ya Serikali kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za viongozi.
“Hili ni wazo la familia ambalo liletwa kwetu kama Serikali nikaona ni zuri na nikaelekeza serikali kulisimamia lakini hili kwetu limetuamsha na kutukumbusha umuhimu wa kuhifadhi historia zetu,” amesema Dk. Samia
Amesema tovuti hiyo itaakisi safari ya maisha halisi ya Dk. Salim lakini pia itatoa fursa ya kutambua historia ya nchi na kuleta shauku ya kujua maisha aliyopitua.
Amesema Dk. Salim alifinya makubwa Afrika na duniani kote ikiwemo kuanzisha baraza la usuluhishi pamoja na kuwa katibu mkuu wa kwanza kwenda Afrika Kusini na kupambana na ubaguzi wa rangi.
“Hizi ni hazina kwa taifa viongozi waliopo na watakaokuja wanapaswa kujifunza ikiwemo uvumilivu kama alivyo Dk. Salim,” amesema Dk. Samia.
Aidha amewataka taasisi ya uongozi kumsaidia Rais wa awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete kukamilisha kitabu chake na kukiweka kwenye tovuti.
Rais Dk. Samia chuo cha diplomasia kwa sasa ni mali ya serikali na amekibadilisha jina na kukiita kituo cha diplomasia Dk Salim Ahmed Salim.
Awali, akimkaribisha Rais Samia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hii ni tovuti ya kwanza kwa kuhifadhi nyaraka za Serikali.
Viongozi waijifunze kwake
Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema mawazo ya Dk. Salim yalizingatia zaidi utaifa hivyo ni wakati wa viongozi kujifunza kupitia maandiko yake mbambali yaliyoko kwenye tovuti.
“Wakati akiwa Waziri Mkuu, Dk. Salim hakuwahi kupendelea upande wowote na mtu ambaye anapenda kusoma vitabu hata ukifika ofisini kwake unakutana na magazeti yote na kuangalia taarifa za habari,” amesema Jaji Warioba.
DK. Salim Ahmed Salim alikuwa Waziri Mkuu wa Tano na Katibu Mkuu wa nane lakini pia alikuwa Mwanadiplomasia mzuri na mwenye mchango mkubwa kwa taifa.