Clara Matimo, Mtanzania Digita- Mwanza
Rais Samia Suluhu Hassan jana Jumanne Juni 16, 2021 amezindua miradi mitatu iliyokuwa ikitekelezwa na Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 60 ikiwemo safari za meli mbili New Victoria Hapa Kazi Tu, New Butiama Hapa Kazi Tu na chelezo ambayo itatumika kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu.
Pamoja na kuzindua safari za meli hizo pia Rais Samia ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli ya mizigo ya bahari ya Hindi, ujenzi wa meli ya abiria na mizigo ya ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli ya kubeba mabehewa ya ziwa victoria, ujenzi wa meli ya mizigo ya ziwa Tanganyika pamoja na mradi mkubwa wa ukarabati wa meli ya kubeba mabehewa ya Mv. Umoja.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamriho, Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu inayofanya safari zake kati ya Mkoa wa Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo Mkoani Kagera imezinduliwa baada ya kufanyiwa ukarabati na serikali, uliogharimu shilingi bilioni 22.7 huku New Butiama Hapa Kazi Tu inayosafiri kati ya Jiji la Mwanza na kisiwa cha ukerewe ukarabati wake ukigharimu shilingi bilioni 4.9. na ujenzi wa chelezo umegharimu Sh bilioni 35.9.
“Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu inauwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo na New Butiama Hapa Kazi Tuinabeba abiria 200 na tani 100 za mizigo,”alisema Dk. Chamriho.
Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa MSCL, Philemon Bagambilana, alisema ujenzi wa Meli hizo tano mpya utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 438.8, utatekelezwa na wakandarasi kutoka Korea ya kusini na wengine kutoka nchini Uturuki.
“Wakandarasi hao ni kampuni ya SM Solution kutoka nchini Korea ya kusini ambao wataifanyia ukarabati meli ya Mv Umoja inayobeba mabehewa na Yutek Gemi ya nchini Uturuki itajenga meli nne,”alifafanua Bagambilana.
Rais Samia aliwataka wafanyakazi na wananchi watakaotumia meli hizo zilizozinduliwa na kuanza safari kuzitunza ili ziendelee kutoa huduma kwa muda mrefu ambapo alibainisha kwamba Miradi hiyo imegharamiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
“Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu bora katika Mkoa wa Mwanza itakayowezesha kukuza biashara ndani ya jiji hili tunataka jiji la Mwanza liwe ni kitovu cha biashara kwa upande wa Afriaka Mashariki.
“Mungu ameuweka mkoa huu mahali pazuri uko kwenye ukanda ambao mikoa yote jirani ni walimaji wa mazoa ya chakula na biashara pia wavuvi wanapatikana hapa ninachosisitiza ni wananchi kutunza miundominu hiyo,”alisema.