23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bei ya pamba yazidi kupaa, wakulima kicheko

Na Derick Milton, Simiyu

Wakati ununuzi wa zao la pamba ukiendelea katika maeneo yanayozalisha zao hilo tangu kuzinduliwa kwake Mei 10, 2021, bei ya zao hilo imeongezeka kutoka bei elekezi ya Sh 1,050 kwa kilo ambayo ilitangazwa na serikali kupitia bodi ya pamba hadi Sh 1,150 hadi Sh 1,200.

Bei hiyo imeongezeka kwa kiwango cha Sh 100 hadi 150 katika maeneo tofauti tofauti ya ununuzi wa zao hilo, ambapo katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu bei imefikia Sh 1,150 na Wilaya ya Meatu mkoani humo ikifikia Sh 1,200.

Kwa mujibu wa bodi ya pamba, imeeleza kuwa ongezeko hilo la bei linatokana na ushindani ulipo kati ya wanunuzi wa pamba kutokana na uhitaji walionao, ambapo kutokana na uwepo wa soko uhuria kwenye zao hilo imesababisha bei kuongezeka.

“Kwetu sisi kama bodi ya pamba tunaweka bei dira ambayo tulitangaza kuwa ni Sh 1,050 ambapo mnunuzi hapaswi kununua pamba chini ya hiyo bei, lakini wanaruhusiwa kupandisha, na hiyo inakuwa furaha kwa mkulima,” amesema Edward Nyawile, Ofisa ufuatiliaji na uhamasishaji Bodi ya Pamba

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga, akitembelea maghala ya kuhifadhia pamba, kuangalia hali ya ununuzi mapema jana na leo amesema wilaya nzima bei imepanda kuanzia jana na kufika 1,150.

Kiswaga amepongeza viongozi wa AMCOS katika maghala aliyotembelea, baada ya kukuta kwenye ubao wamebandika bei mpya, ambapo alizitaka Amcos zote wilayani humo kuhakikisha mkulima anauza pamba kwa bei hiyo mpya.

Amesema kuwa serikali Wilayani humo itahakikisha inafuatilia kila mara kuongezeka kwa bei ili wakulima waweze kunufaika na zao hilo, huku akisisitiza uwepo wa ufuatiliaji kuona kama kweli wakulima wanalipwa pamba yao kwa bei ya ongezeko.

“Tutafanya ufuatiliaji wa kila siku kuona kama kweli wakulima wanalipwa kwa bei mpya na siyo ile ambayo ilitangazwa na serikali mwanzoni, niwape onyo viongozi wa Amcos wenye nia hiyo waache mara moja,” amesema Kiswaga.

Aidha, Kiswaga amewataka watu wote ambao wananunua pamba kwa njia za panya (machinga) na kuwataka waache mara moja kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kutaifishwa kwa pamba ambayo watakutwa nayo.

Wakulima Kicheko

George Mabula ambaye ni mkulima wa Byuna, ameishukuru serikali kwa ongezekezo hilo kwani linawapa hamasa ya kuongeza eneo la kuzalisha kwa zao hilo zaidi msimu ujao.

Mabula mesema anatamani kuona bei hiyo ikiongezeka zaidi ili wakulima wengi waweze kunufaika kwa kujikwamua kupitia jasho lao hilo.

“Kama unavyojua kwamba wakulima tunatumia gharama kiubwa sana katika kuhakikisha kuwa tunazalisha pamba iliyobora zaidi, hivyo kuendelea kuimarika kwa bei itakuwa ni fursa wetu ya kufanya maendeleo,” amesema Mabula.

Katika msimu uliopita wa ununuzi wa zao hilo 2019/20 bei iliyotangazwa ilikuwa Sh 810 kabla ya kuongezeka na kufikia Sh1,000, ambapo uzalishaji nao umeongezeka kutoka tani 122,650 msimu uliopita na kufikia tani 393,000 msimu huu ongezeko la asilimia 68 ya uzalishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles