Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, mkoani Mwanza imeanza leo kwa hamasa kubwa, ikilenga kuimarisha maendeleo ya mkoa huo na kutoa fursa kwa wananchi kuwasilisha changamoto wanazokabiliana nazo moja kwa moja.
Katika ziara hii, Rais Samia atapata nafasi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miundombinu ya barabara, sekta za afya, elimu na uwekezaji. Vilevile, atatoa maelekezo mahsusi ya kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo ili kufikia malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ziara hii pia itakuwa jukwaa muhimu kwa Rais Samia kuzungumza na wananchi na kuhamasisha ushirikiano wa karibu kati ya serikali na jamii katika kukuza uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, hotuba zake zinatarajiwa kugusia masuala ya kisera, akisisitiza umuhimu wa utulivu na amani kama nguzo za msingi katika safari ya maendeleo ya taifa.