27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia atoa bil. 300 kuendeleza miradi Dodoma

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa sh.300 bilioni ya kuendeleza ujenzi wa Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Agosti 13, baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Ikulu mpya Chamwino, Dodoma ambao umefikia asilimia 78.

“Rais Samia amedhamiria kuendeleza miradi yote ikiwamo ya ujenzi wa makao makuu na miradi mbalimbali inayofanyika hapa Dodoma. Hatua hii ni uthibitisho tosha kwa Watanzania kuwa kazi zinaendelea.

“Ujenzi wa Makao Makuu bado unaendelea, Rais Samia ameelekeza kazi zote ziendelee zikiwemo za ujenzi wa mji wa Serikali hapa Dodoma,” amesema Majaliwa.

Amesema kuwa kati ya fedha hizo, bilioni 131 zitatumika katika ujenzi wa majengo ya magorofa ya makao makuu ya wizara kwenye Mji wa Serikali, Mtumba.

Aidha, Waziri Mkuu amesema bilioni 169 zitapelekwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa  maboresho ya jiji hilo ikiwamo miundombinu ya barabara, maji na umeme.

Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akutane na mawaziri wenzake ili waanze mchakato wa ujenzi majengo ya wizara.

“Ujenzi huo unatakiwa uanze Septemba, mwaka huu na ufanywe na kampuni za ukandarasi za Serikali pamoja na kampuni za sekta binafsi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo na hatua iliyofikiwa na kwamba ana imani utakamilika kwa wakati.

“Leo nimefarijika kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huu na furaha hii inatokana na hatua tuliyoanzia na tulipofikia sasa. Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli alitaka kuona Ikulu mpya inafanana na ya Dar es Salaam na leo nimeona kweli zinafanana.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles