Na Mwamdishi Wetu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha Taifa linabaki kuwa moja na salama, hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kuwa macho katika kipindi chote cha uchaguzi kuanzia wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024 hadi uchaguzi mkuu mwakani.
Ameyasema hayo leo Septemba 17,2024 wakati akizunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Polisi pamoja na kuhitimisha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi, mkoani Kilimanjaro.
Amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linamchukulia hatua na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria yeyote anayejaribu kuhatarisha amani ya nchi kwa kisingizio cha uchaguzi.
“Uchaguzi utapita lakini Tanzania itabaki, tunataka kubaki na Tanzania yenye usalama, na Tanzania yenye utulivu ili shughuli za maendeleo ziweze kuendelea, hivyo nalitaka Jeshi la Polisi kuwa macho kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” amesema Rais Samia.
Aidha amelitaka jeshi hilo kupeleka mkakati wa kupambana na utapeli wa mtandaoni na kuona namna ya kufanya ili kuliwezesha jeshi kukabiliana na hali hiyo.