Na Clara Matimo, Mwanza
Umoja wa Machifu Tanzania(UMT) leo umemsimika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa chifu Mkuu wa Tanzania na wamempa jina la hangaya lenye maana ya nyota angavu.
Zoezi hilo la kumsimika kuwa Chifu Mkuu wa Tanzania limefanyika katika uwanja wa msalaba mwekundu(ngomeni) uliopo wilaya ya Magu Mkoani Mwanza baada ya kumaliza kuhutubia machifu na mamia ya wananchi waliofurika uwanjani hapo kwenye kilele cha tamasha la utamaduni mila na desturi zetu lililoandaliwa na UMT.
Akizungumza wakati akimsimika uchifu Rais Samia Suhulu Hassan, Mwenyekiti wa Umoja wa Watemi wa Usukuma, Itale Charles, amesema nyota angavuni nyota ya asubuhi ambayo inangaa alfajiri kabla ya jogoo kuwika kwa mara ya pili inayohimiza watu kuamka na kwenda kuwajibika.
“Ni nyota inavyoashiria matumaini, kama ambavyo wewe rais wetu umekuwa na matumaini makubwa kwa watanzania na watanzania tunamatumaini makubwa na wewe, tumekupa jina hili kwa kutambua mchango wako katika kusimamia na kuthamini utu wa wanyonge na utamaduni wetu,”amesema Chifu Itale.
UMT wamemkabidhi Chifu Mkuu wa Tanzania, Rais Samia vitu mbalimbali
Nguo nyeusi ambayo ni alama ya mawingu meusi yanayoleta mvua watu wanalima na kupata chakula hivyo wamemtaka awe baraka kwa watanzania, nguo nyekundu, ngao na mkuki vinawakilisha alama ya ulinzi avitumie kama silaha kulinda nchi yake pamoja na ngozi ya chui kwa kuwa ni mnyama mpole lakini ni mlinzi hodari kwa watoto wake wamemtaka awe mpole kwa watanzania wote lakini mwangalifu kwa wanaotaka kuwadhuru wananchi wake au nchi yao.
Pia wamemvisha ushanga uliotengenezwa kwa ganda la yai la mbuni maana ni ndege pekee aliyemwangalifu sana kwa vifaranga vyake anaweza hata kupigana na wanyama wakali kama fisi ili kuwalinda watoto wake wasiweze kupata madhara na yeye watanzania ndiyo vifaranga vyake wamemuomba awalinde na kuwalea.
Usinga ukiwakilisha watanzania kama ambavyo mtu hawezi kuhesabu singa kutokana na wingi wake hivyo naye ana watu awatumie kuleta maendeleo ya nchi akawalinde, kiti cha kiutawala chenye mguu mmoja kikimaanisha yeye ndiye chifu mkuu hakuna mwingine akitumie kukaa na kuwasikiliza wananchi wake wazungumze na kupata muafaka wa mambo mbalimbali watakayoyajadili.
Chifu Mkuu wa Tanzania atoa neno baada ya kusimikwa
Akizungumza baada ya zoezi la kusimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Tanzania kukamilika, Rais Samia ameahidi kushirikiana na machifu wote nchini kuendeleza tamaduni mila na desturi za watanzania kwa faida ya vizazi vijavyo.
“Nawashukuru sana UMT kwa kunipa jina hili zuri namuomba Mungu anisaidie nising’are peke yangu ning’are na wananchi wangu pamoja na nchi yangu naahidi kushirikiana nanyi katika kuhakikisha tamaduni zetu tunazilinda,”amesema.
Awali Mratibu wa Tamasha hilo, Chifu Aron Mikomangwa Nyamilonda wa III akisoma hotuba ya UMT mbele ya Rais Samia, ameiomba serikali kuwatambua rasmi na kuwapa usajili waungane na serikali kulinda utamaduni wa nchi, eneo la ardhi makao makuu Dodoma kwa ajili ya kuweka ofisi na miradi itakayowezesha umoja huo kujiendesha kiuchumi.
“Pamoja na maombi hayo mheshimiwa rais tunakabiliwa na changamoto mbalimbli ikiwemo kupoteza umiliki wa majengo yetu, upatikanaji wa nyara za serikali kwa ajili ya kuzitumia kwenye shughuli zetu za kila siku, ubovu wa miundo mbinu kwenye vituo vya makumbusho na kuvamiwa kwa maeneo ya himaya za jadi.
“Vituo vingi vya makumbusho vinahitaji kuboreshwa kufikia kiwango cha kimataifa hata vile visivyopokea ruzuku kutoka serikalini mfano miundombinu ya majengo katika kituo cha makumbusho cha bujora ni mibovu hicho ni kituo pekee duniani kinachoonyesha utamaduni halisi wa kabila la wasukuma na watanzania.
“Tunaomba ukiboresha kituo hicho kitakuwa ni kituo bora kitakachouinua utamaduni wetu, tunaomba uwanja huu wa ngomeni ambapo tamasha hili linafanyika urudi kwa waasisi ambao ni wananchi wa eneo hili na machifu,”amesema.