Mwandishi Wetu, Dodoma
Juni 23 ya kila mwaka katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU), hufanyika tukio kubwa kwa nchi wanachama wa umoja huo.
Tukio hilo ni Siku ya Utumishi wa Umma Afrika ambayo ni mahususi katika kutambua, kutoa tuzo na kuthamini mchango wa watumishi wa umma katika kuleta maendeleo katika nchi zao.
Tanzania ni moja ya vinara wa Siku ya Utumishi wa Umma Afrika kwani tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 tukio hili linafanyika, na vilevile kwa ngazi ya Bara la Afrika kwa kuwakutanisha pamoja nchi wanachama wa AU na kutoa tuzo za kutambua mchango wao katika utumishi wa umma, tukio hilo limefanyika mara mbili.
Siku hii hutanguliwa na matukio mbalimbali ikiwamo kuonyesha ubunifu na maboresho ya kazi zilizofanywa na watumishi wa umma katika kuleta maendeleo ya wananchi. Ni jambo lisilo na mjadala kuwa wananchi ndio wadau wakuu wa Serikali.
Ni wazi kuwa Utumishi wa Umma ndio injini ya kuendesha shughuli za Serikali kwa jamii hivyo, Siku ya Utumishi wa Umma hutumika kupokea mrejesho kutoka kwa watumishi wa umma pia na wadau mbalimbali wa huduma zinazotolewa na Serikali ili kuboresha au kufanya ubunifu zaidi katika kutoa huduma.
Hapa Tanzania sekta ya maji haipo nyuma katika muktadha mzima wa AU katika kuangalia mafanikio na kung’amua changamoto katika utoaji wa huduma.
Watumishi na viongozi wake wanapambana katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kupitia huduma ya maji ambayo ni chachu ya kuimarisha huduma nyingine katika jamii.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amejionea mabadiliko na mapinduzi yanayofanyika katika sekta ya maji hapa nchini.
Kazi kubwa inayoendelea ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, mabadiliko haya yanafanikishwa na watumishi wa umma katika Sekta ya Maji.
“Hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza. Wizara ya Maji si wizara ya ukame,” ni moja ya nukuu ya viongozi wa Wizara ya Maji katika mihadhara na kazi mbalimbali wanazozishiriki pamoja na umma wa Watanzania.
Hilo limejidhihirisha mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi ya Rais Samia ambapo moja ya kazi aliyofanya ni uzinduzi wa mradi wa maji wa Misungwi wenye thamani ya Sh bilioni 13.77. Mradi huo umetekelezwa na Serikali na wabia wa maendeleo.
Rais Samia akiongea na maelfu ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo uliofanyika wilayani Misungwi aliwataka kulinda miundombinu ya maji iliyojengwa hapa nchini kwa sababu serikali inaingia gharama kubwa kuitekeleza ili kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa jamii.
“Naiagiza wizara na wahandisi wa mkoa na wilaya hapa Mwanza kuhakikisha maji yanasambazwa kwa kasi ili yawafikie wananchi wote,” Rais Samia anasema na kuongeza mazingira yalindwe ili kulinda vyanzo vya maji.
Anawaasa wananchi wajenge tabia na utaratibu wa kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabwawa na visima ili kumaliza tatizo la maji nchini.
Rais Samia pamoja na kuzindua mradi huo amewataka wananchi kulipa bili za maji ili huduma hiyo iwe endelevu na kufikishwa kwa wananchi wengine na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kutokubambikiza wateja bili za maji bali kila mmoja alipe bili kuendana na matumizi halali. Anasema ulipaji wa bili kwa wakati utawezesha kujengwa kwa miradi mingine ya maji hapa nchini.
Wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametumia wasaa huo kwa kuwaambia wananchi kuwa mageuzi yanayofanyika katika sekta ya maji yamepania kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.
Aweso anasema jambo la msingi ni kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Samia ili dhamira ya kuleta maendeleo kwa wananchi itimie kama ilivyopangwa.
“Maji ni uhai na maji hayana mmbadala kwa mfano si kama chakula kwamba ukikosa wali basi utakula ugali…anayejua mihemo ya mgonjwa ni yule aliyelala naye, hivyo mipango yote ni kuhakikisha maji yanatoka bombani na kuondoa kero kwa kina mama na jamii kwa ujumla,” anasema Aweso.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, akiuzungumzia mradi wa maji wa Misungwi anasema mradi wa maji wa Misungwi una uwezo wa kuzalisha kwa siku lita za maji milioni 4.5 na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi 64,000 wa Misungwi na maeneo jirani, ambapo mradi huo umeongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 42 hadi kufika asilimia 83 kwa eneo la Misungwi mjini. Mradi wa Maji wa Misungwi una mabomba yenye urefu wa kilomita 57.14.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, anasema kuwa wastani wa upatikanaji wa huduma ya majisafi mkoani Mwanza ni asilimia73 na hali hiyo inazidi kuimarishwa ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
Waziri Aweso akiongea na wananchi hivi karibuni kuhusu kazi ya kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi, anasema kuwa Serikali ilianzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) unaohusika katika ujenzi wa miradi na usimamizi wa huduma ya maji vijijini.
RUWASA imerithi miradi yote ya maji ikiwemo miradi ya maji ya vijiji 10 iliyokuwa inatekelezwa chini ya halmashauri za wilaya.
Anasema baadhi ya miradi ya maji iliyorithiwa imekuwa na changamoto ya kutokamilika kwa wakati na mingine kukamilika bila kutoa maji, na jumla ya miradi 177 ilibainika kuwa na changamoto hizo ambapo hadi kufikia Machi 2021, miradi 85 ilipatiwa ufumbuzi na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
“Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na miradi ya maji ya Ntomoko (Dodoma), Nyamtukuza (Geita), Mibono (Tabora), Rugeye (Mwanza), Malinyi ( Morogoro), Muze group (Rukwa), Kinesi ( Mara) na Imalabupina-Ichwankima (Geita).
“Kazi ya ukwamuaji wa miradi hiyo unaendelea kwa kutumia timu maalumu za wataalam zilizopewa jina maarufu kama ‘Water Rescue Teams’,” anasema Aweso.
Anasema mapinduzi na mageuzi makubwa yaliyojiri katika sekta ya maji ni pamoja na kuzinduliwa kwa miradi mikubwa ya maji ya Tabora – Igunga – Nzega pamoja na Isaka – Kagongwa baada ya kazi kubwa ya utekelezaji wake kukamilika.
Utekelezaji mwingine ni kukamilika kwa miradi ya maji 422 ambapo kati ya hiyo vijijini ni miradi 355 na mijini miradi 67; kuanza kutoa huduma ya maji kwa miradi 85 iliyokuwa na changamoto ya kutotoa huduma kwa muda mrefu; kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na kupungua kwa gharama za ujenzi kutokana na kutumia utaratibu wa force account ambapo zaidi ya miradi 150 imetekelezwa.
Aweso anaongeza kuwa mageuzi makubwa ni pamoja na idadi ya maabara za ubora wa maji zenye ithibati umeongezeka kutoka maabara moja hadi kufikia saba. Maabara hizi hutumika kupima ubora wa maji na kwa kupata ithibati zimefikia kiwango cha kimataifa.
Kwa ujumla hapa nchini hali ya huduma ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini na mijini hadi kufikia Machi, 2021 kwa vijijini ilikuwa wastani wa asilimia 72.3 kutoka wastani wa asilimia 70.1 Machi, 2020. Kwa upande wa mijini hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi imeongezeka kutoka asilimia 84 Machi, 2020 hadi asilimia 86 Machi, 2021.
Pamoja na takwimu hizo Tafiti zilizofanywa na Wizara ya Maji mwaka 2019 zimeonesha kuwa rasilimali za maji zinazoweza kupatikana kwa mwaka kwa matumizi mbalimbali hapa nchini ni wastani wa mita za ujazo bilioni 126. Kati ya hizo, mita za ujazo bilioni 105 ni maji juu ya ardhi na mita za ujazo bilioni 21 ni maji chini ya ardhi.
Kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 55.9 kwa mwaka 2019, kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,250. Kiasi hicho ni juu ya wastani wa mita za ujazo 1,700 ambacho ni kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa.
Kama ilivyoelezwa na viongozi mbalimbali na Rais Samia kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ni jukumu la kila mwananchi ili rasilimali maji iendelee kuwepo kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Utunzaji wa vyanzo vya maji utahakikisha uhakika wa huduma za maji katika miradi na matumizi mengine ya maendeleo.