26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aipongeza Wizara ya Madini kwa usimamizi madhubuti wa sekta

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Hassan ameipongeza wizara ya madini kwa usimamizi mzuri na madhubuti wa sekta ya madini unaopelekea ukuaji wa haraka na kuwa kinara katika kuchangia kwenye Pato la Taifa.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 13, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati akifunga maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Aidha, Mh Rais Samia ameeleza katika mikakati ya kuimarisha uchumi wa nchi na upatikanaji wa fedha za kigeni Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetenga kiasi cha shilingi Trilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji.

Rais, Dt. Samia amesema kwamba sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa katika kuliingizia taifa fedha za kigeni ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilichangia asilimia 56 ya fedha za kigeni.

Sambamba na hapo Rais Dk. Samia amesema kiasi cha Sh bilioni 250 zimetengwa kama dhamana ya mikopo zitakazo wawezesha wanunuzi wa dhahabu kupata mtaji.

Rais Dk. Samia ameongeza kuwa, kwa mwaka wa 2023 mauzo ya madini yenye thamani ya zaidi ya sh trilioni mbili yaliuzwa katika masoko 44 na vituo mbalimbali vya uuzaji madini vilivyopo sehemu mbalimbali nchini.

Akielezea kuhusu mwenendo wa biashara ya madini nchini kuanzia mwaka 2019 mpaka septemba 2024 , Dk. Samia amesema kwa kipindi husika kiasi cha tani 20.8 za dhahabu zenye gharama ya sh trilioni 5.2 zimenunuliwa kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini nchini.

Dk. Samia ameeleza kwamba serikali inatambua mchango wa asilimia 40 kutoka kwa wachimbaji wadogo nchini, ambapo ametoa leseni 21 kwa vikundi vya Vijana na wanawake vikiwemo vikundi vya GEWOMA, Ushirika Madirisha na TEWOMA vinavyojihusisha na uchimbaji mdogo.

Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko ameipongeza wizara ya madini kwa juhudi mbalimbali inazofanya za mageuzi katika mnyororo wa thamani madini hususan katika masuala ya uongezaji thamani madini na mpango wa kufanya utafiti wa kina kwa asilimia 50 ifikapo mwaka wa 2030.

Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ndani ya sekta ya madini, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema katika kuimarisha uchimbaji wenye tija na uhakika Serikali itajenga Maabara kubwa mkoani Dodoma na Geita ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupeleka sampuli zao kwa ajili ya uchunguzi.

Waziri Mavunde amesema kuwa, wizara inaendelea kuweka mipango mizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ambapo kwa kipindi cha siku 90 cha mwaka wa 2024/2025 wizara kupitia Tume ya Madini imekusanya kiasi cha Sh Bilioni 287 ambayo ni zaidi ya asilimia 106.

Akielezea kuhusu utekelezaji wa Sheria na Kanuni ndani ya Wizara, Waziri Mavunde amesema kuwa wizara imekuwa ikizingatia taratibu zote za utekelezaji wa Mpango wa Ushirikishwaji wa Jamii inayozunguka mgodi na Mpango wa Urudishaji kwa Jamii ambapo kwasasa ipo na mpango mpya wa Mining for Brighter Tommorrow (MBT) utakao washirikisha vijana na wakina mama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo mkoani Geita katika sekta ya Afya,Maji, Barabara na Elimu.

Pamoja na mambo mengine, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wadogo wa madini Tanzania (FEMATA) John Bina amemuomba Rais Dk. Samia kuifanya dira ya Vision2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri kuwa kitaifa badala ya kisekta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles