Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), kuweka mkakati wa kushughulikia changamoto ya udanganyifu wa mitihani nchini ili wahitimu wafaulu kwa haki.
Maagizo hayo ameyatoa leo Desemba 16,2023 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya NECTA, jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa utanganyifu unasababisha kuzalisha watu wasio na tija kwa Taifa.
“Sasa kuna wahitimu mamilioni, tunapowachukua ndani ya ajira ukiwapa kazi ndogo akufanyike hawawezi, unajiuliza huyu kaja na cheti chake, katoka chuo, kwa hiyo tunazalisha nguvu kazi ambayo haipo ‘productive’ ,haina tija kwa taifa, lazima tujitazame katika utungaji wa mitihani na usahihishaji, kubwa zaidi udhibiti wa mitihani.
Tukitoa mianya ya watoto wetu kufanya mitihani kwa kuijua kabla tutatoa ‘product’ isiyokuwa nzuri, tuzingatie hilo ili tutoe nguvu kazi nzuri itakayotumika vyema katika maeneo mbalimbali,”amesema.
Pia ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme kuwawezesha wanafunzi waliopo pembezoni kujifunza na kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa njia ya mtandao.
Rais Dk.Samia amesema serikali itaendelea kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi wa sayansi wasiokuwa na walimu wa kutosha kusoma kwa kutumia teknolojia.
“Kutokana na watahiniwa wote kutahiniwa sawa bila kujali mazingira na changamoto yoyote, serikali itaendelea kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi hasa wa sayansi ambao hawana walimu wa kutosha ,wasome kwa kutumia mfumo wa kimtandao unaotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF),” amesema.
Amesema mfumo huo umekuwa na matokeo chanya kutokana na wanafunzi wanaoutumia kufanya vizuri katika masomo yao.
Rais Dk. Samia amesema mfumo huo umesaidia kupunguza gharama ya kununua vifaa vya maabara kwa wizara kwani mwanafunzi anaviona katika mtandao na anaweza kufanya mtihani au kusoma kwa mtandao.
Amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Tehama ambao umeimarisha utendaji wa Baraza hasa katika matumizi ya teknoliojia katika usajili wa watahiniwa, uchapaji, usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.
“Serikali tutaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu kuhakikisha ufundishaji , usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia,” amesema.
Amezitaka a NECTA kutekeleza majukumu yao kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususani katika upimaji umahiri.
Amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa Baraza hilo kulingana na mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana nalo kufikia malengo ya muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapishaji kadri uwezo utakaporuhusu.
“Kutokana na kukua kwa teknolojia siku hadi siku mitambo ya uchapishaji inapoteza ubora wake hivyo ili kuongeza ufanisi katika Baraza la Mitihani, serikali itaongeza mtambo mmoja kila mwaka kuliwezesha baraza kuendelea kuboresha huduma zake kupitia teknolojia,” amesema.
Ameeleza kuwa NECTA imeomba kuongezewa mitambo mitatu na mmoja unagharimu sh. bilioni sita, hivyo ameahidi kuanzia mwaka wa fedha ujao kuona namna ya kuwapa mtambo mmoja kwa kila mwaka.
Naye Spika wa Bunge, Dk.Tulia Akson amelipongeza baraza hilo kwa kutimiza miaka 50, kwani ni muda muafaka wa kutafakari lilipotoka, lilipo sasa na linapokwenda.
Amesema bunge litaendelea kutoa ushirikiano kwa kulisimamia na kulishauri baraza hilo kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
“Rais Dk.Samia kwa miaka hii 50 tunaomba kuangalia namna ya kuweka mazingira yanayofanana kwa wanafunzi wote kwa sababu wanatahiniwa sawa,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ndani ya miaka 50 ya NECTA, wamefanikiwa kudhibiti wizi wa mitihani ukilinganisha na nchi nyingine.
Amesema katika mtihani uliofanyika hivi karibuni wamebaini majaribio ya wizi lakini hayakufanikiwa kwa sababu yalidhibitiwa mapema kwa kuwa wakali.
“Kwa yoyote atakayejaribu kuiba mitihani hasa kwa mfumo wa taasisi tutamchukulia hatua kali kwa sababu Baraza la Mitihani liko macho kila kukicha,” amesema.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohomed ametoa pole kwa waathirika wa mafuriko wilayani Hanang, mkoani Manyara ambapo baadhi ya wananchi walipoteza vyeti vyao vya elimu hivyo aliahidi kuwa Baraza litatoa mbadala.
Hata hivyo amesema Baraza hilo limejikita kuwekeza zaidi katika Tehama kwa kutoa elimu kwa njia ya mtandaoni.