MOSCOW, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, amemtumia ujumbe wa salamu za pongezi mwenzake wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, kwa taifa hilo kutimiza miaka 70 ya kuanzishwa kwake.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), Rais Putin alituma salamu hizo za pongezi jana kwa njia ya telegram akieleza kuwa ana uhakika mataifa haya mawili yataendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali.
Shirika hilo lilieleza kuwa katika salamu hizo, Rais Putin alielezea pia kwamba ana uhakika Serikali za Moscow na Pyongyang zitafanya mazungumzo ya kimataifa yatakayosaidia kujenga ushirikiano zaidi katika nyanja hizo mbalimbali.
“Nakupongeza kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 ya  kuanzishwa Jamhuri ya Demokrasi ya Watu wa Korea Kaskazini, DPRK. Nasema tuna uhusiano mkubwa na wa kuridhisha baina ya Serikali ya Urusi na DPRK,” Shirika hilo la KCNA liliukariri ujumbe huo.
“Uhusiano huu unatimiza kikamilifu masilahi ya watu wa nchi zetu na unasaidia kuimarisha hali ya utulivu na usalama kwenye Peninsula ya Korea na Kaskazini na bara kwa ujumla,” uliongeza ujumbe huo.
Shamrashamra za maadhimisho hayo ya miaka 70 zilifanyika jana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Pyongyang na kuhudhuriwa na viongozi kutoka mataifa mbalimbali ambapo Urusi iliwakilishwa na Spika wa Bunge, Valentina Matviyenko.