27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Rais Magufuli hatutaki ufe

raisNENO la kuwa yuko tayari kufa! Kuwa anautoa mwili wake sadaka! Kuwa yuko tayari kurudi kijijini akachunge ndege au ng’ombe, na kadhalika limekuwa likijitokeza mara kwa mara kwenye matamko ya Rais John Magufuli.

Ni maneno mazito kutoka kwa Rais wa nchi na yanaleta ujumbe mzito sana. Mimi ninasema kuwa hatuhitaji kusikia Rais wetu amekufa. Nakumbuka wosia kutoka kwa Mwandishi wa riwaya ya Kiingereza ya Pretorian Agenda, Peter Msechu, kuwa kufa ni hasara na kuwa kufa kunatupotezea mtu na kubaki hai ndio iwe juhudi ya kila mtu, kwani utaendelea kuwa wa faida. Tunakuhitaji JPM uendelee kuwa hai na kuongoza juhudi hizi za kulisafisha taifa na uchafu ambao kwa kweli unatia aibu.

Unapoona maelfu ya vijana wa kiafrika kule Bahari ya Mediterranean wakizama na kufariki wakizikimbia nchi zao, ni wazi kuwa sababu ni kuwakimbia viongozi wa Afrika ambao kwa miaka yote wamekuwa wakitumia madaraka kujinufaisha wao na wa kwao.

Ni jambo la kutia aibu kwa Afrika. Kwa hiyo kwa juhudi zako JPM na kwa kusema kuwa Taifa hili ni tajiri kiasi kwamba lingeweza kuwa hata mfadhili kwa nchi zingine masikini, inaonyesha kuwa wale waliokutangulia hawakuwa wakifikiria kwa msingi huo. Unaenda kinyume nao na kinyume na fikra za viongozi wengi wa Afrika. Na tunajua fikra zako zinawaudhi watu.

Kuna wanaochambua matamshi yako wakisema kuwa unataka kutumia kisingizio cha kutishiwa maisha ili uweze kutimiza ajenda yako ya kidikteta. Ukavunja sheria za nchi na Katiba. Mimi sifikirii hivyo, Rais ni mtu mkubwa sana katika taifa, anapotamka jambo neno lake linapaswa kupewa fursa ya tafakari. Rushwa iliota mizizi.

Rushwa ilijenga mtandao ndani na nje ya Serikali; ndani na nje ya nchi. Rushwa ilikuwa ikisababisha watu kupata mabilioni bila kufanya kazi; rushwa iliwapeleka watu kwenye madaraka ya ubunge, ukuu wa wilaya au ukuu wa mkoa na uwaziri, rushwa ilisababisha watu kuajiriwa bila vyeti sahihi au vyeti halali; rushwa ilisababisha watu kulikosesha taifa fedha za kodi.

Rushwa ilisababisha taifa kuingia mikataba feki ya ndani na nje na kusababisha nchi kupata hasara; Rushwa ilisababisha nchi kushindwa kuendesha mashirika yake yenyewe.

Litania ya madhara ya rushwa ni ndefu na ikawajenga watu kuwa miungu, walikuwa wakilindwa na vyombo vyetu wenyewe ambavyo viliundwa kulinda maslahi ya taifa na wananchi, vikawa vikaragosi vya watu mafisadi.

Rais anapotaka kutibua mtandao huo, haliwi ni jambo la kufurahisha kwa waliokuwa wakiishi kwa mtindo huu. Ukisikia habari za ndani ya jinsi watu mafisadi walivyokuwa wakiikamua nchi hii na kuyapata maziwa na asali bila jasho, utaona kuwa tamko la Rais la kuwa yuko tayari kujitoa sadaka linaakisi nguvu kubwa anayopigana nayo.  Watu waliokamatwa na sukari kwa mfano, tena mfano tu wengine tunawafahamu kwa zaidi ya miongo mitano. Tunajua nguvu zao, tunajua walivyokuwa wakishirikiana na walio ndani ya Serikali… nilipokuwa mwandishi wa habari… tena bado mchanga kabisa… mhariri wangu alinituma kwenda mahali fulani, tena ofisi ya Serikali kuulizia kitu ambacho ni cha kawaida tu lakini asubuhi mwandishi wa habari mwenzangu aliyekuwa katika mtandao fulani alikuja na kuniuliza ulikwenda mahali fulani kuulizia jambo fulani na huyo unayemwulizia anakuuliza unamtafuta nini.

Ilikuwa siri yangu na Mhariri wangu, nikagundua kuwa kule nilikokwenda kumwuliza alikuwa ameweka mashushushu wake ambao walikuwa wakimtajia kila mtu anayekuja kuulizia habari zake.

Lakini kuna siku nilikuwa nikifuatilia habari za wizi wa mafuta kule kurasini, watu walikuwa wakinyonya mafuta kwenye bomba na kuondoka nayo… tulifuatilia… tukagundua ni nani alihusika lakini tukagundua kuwa wakati mafuta yakinyonywa kulikuwa na ulinzi mkali “halali”— hahaha—“ulinzi halali”…. Na tulipokwenda kuulizia mahali husika hatujapata majibu hadi kesho.

Nchi ilikuwa imeanza kujibainisha kama nchi ya watu wachache wenye kumiliki kila idara kwa fedha zao na kwa kujitengenezea mtandao hivi karibuni nilisikia habari za kunitisha… na ni za kweli… kijana dereva wa malori aliambiwa kuna kazi ya siku moja tu… ya kuleta mzigo bandarni kutoka mahali fulani…. Akapelekwa kwenye yadi kubwa ya malori… akaambiwa panda… na pembeni akapanda mtu aliyevaa nguoa za idara fulani ya usalama… inawezekana alikuwa usalama feki… lakini alitaka kuleta hali ya kuonyesha kuwa ati ule mzigo ulikuwa nyeti kwa serikali…. Ukafika bandarini. Ghafula akatokea mtu fulani… naomba nisitaje jina… akaukagua mzigo wake, akamlipa dereva fedha, si haba, kwa kazi ya siku moja…lakini alishangaa.. kumbe nchi ndivyo ilivyo. Kama sisi watu wa kawaida tunayajua machache haya, je Rais mwenye masikio na macho kila kona anajua mangapi mazito, anayajua mangapi yanayohusu hasira za anaowatibulia mipango yao. Tamko la kuwa mniombee, kutoka kwa Rais si tamko la mchezo… si tamko la kutaka sifa au huruma… ni tamko la mpiganaji mpweke kati kati ya maadui ambao wana mitandao na wenye ushirika mpana.

Lakini nilitaka nimalizie kwa kusema kuwa haya yalianza baada ya chama chako mwenyewe kuona kuwa ufisadi, wenyewe wakiita “takrima” kuwa ni sehemu rasmi ya maisha nje na ndani ya siasa. Nje na ndani ya serikali. Kuwa ukiwa kiongozi unakuwa na uhalali wa kuishi kwa kuvunja sheria. Na kwa kweli ilifika mahali hata madiwani walikuwa juu ya sheria—waliweza kuuza viwanja vya umma na kupindisha sera na sheria kwa ajili ya faida binafsi.  Haya yote ambao rais anayaibua kama madudu, majipu, yalitokana na sera ya kulindana. Ya kukifanya chama kuwa kama kamati ndogo ya kulinda maovu yanayofanywa na wanaserikali. Na kwa sababu hao wanaserikali walikuwa na nguvu sana na waliwatishia wabunge wabishi kutopata tena uongozi, basin chi ikaona ufisadi ni sehemu muhimu yamaisha nje na ndani ya siasa. Hakuna aliyekuwa akijali kuona tembo wanapotea, madini hayaleti faida, bandari inakosa tija, mikataba feki inatengenezwa, na nchi inashindwa kulipa hata mishahara yake kutoka kwenye vyanzo vya serikali ila kwa kukopa na kuongeza deni. Utakapokuwa mwenyekiti wa Chama, kama wakikuachia, basi tafadhali anza na kuwabadilisha hawa wa kwako- chama chako, kuwasafisha kifikra. Kuwa nchi haiendi kwa kuwakumbatia mafisadi bali kupigana nao. Narudia tena hatuhitaji ufe… utatuletea hasara! Tunajua unaweza kujilinda… na tutawalaumu wale waliopewa jukumu la kukulinda….wakishindwa kukulinda katika harakazi hizi maridhawa unazoziendesha!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles