Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amesema viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa ya kuhubiri amani, umoja na mshikamno, hivyo Watanzania wana kila sababu ya kuwaunga mkono.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kuungana na waumini wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano alipokwenda kusali ibada ya Jumapili.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo baada ya kumalizika ibada, Rais Dk. Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli aliwashukuru viongozi na waumini wa Kanisa la Anglikana na madhehebu mengine ya dini kuendelea kuliombea taifa na kudumisha amani na utulivu.
Alisema viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.
“Ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuliombea taifa hili, ninawashukuru kwa sababu siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele, ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo udumu ndani yetu sisi sote.
“Makanisa yote, madhehebu yote, dini zote, vyama vyote, upendo tukiujenga ndiyo tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Kwa upande wake, Padre Jackson Sostenes aliyeongoza ibada hiyo alimshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kuungana na waumini wa kanisa hilo na kuahidi viongozi na waumini wa kanisa hilo wataendelea kumwombea na kuliombea taifa.
Katika ibada hiyo, Rais Dk. Magufuli alitoa Sh milioni moja kuchangia vikundi vya kwaya vya kanisa hilo.