Mwandishi wetu-Dar es Salaam
RAIS John Magufuli ameadhimisha miaka 56 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa kutoa msamaha kwa wafungwa 3,973 kati yao, 256 wakiwa ni waliohukumiwa kunyong’wa hadi kufa na sasa wamebadilishiwa adhabu.
Taarifa kwa umma iliyotolewa jana Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli alitoa adhabu hiyo akiwa Chato mkoani Geita.
“Katika kuadhimisha miaka 56 ya muungano, Rais Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,973 ambapo kati yake wafungwa 3,717 wamesamehewa vifungo vyao, na wafungwa 256 waliokuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa hadi kufa wamebadilishiwa
“Rais Magufuli amesema ana matumaini kuwa wafungwa hao wamejifunza na watajirekebisha ili waungane na jamii katika kulitumikia taifa wakiwa raia wema wanaozingatia sheria na taratibu,” ilisema taarifa hiyo.
Desemba 2017, Rais mMagufuli aliwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa.
Hata hivyo idadi ya wafungwa wengine walioachiwa huru kutokana na makosa mbalimbali walikuwa 1,821, huku wengine 8157 wamepunguziwa adhabu zao.
Rais Magufuli alikwisha weka wazi msimamo wake juu ya utekelezaji wa hukumu ya kifo, akisema hawezi kusaini mfungwa yeyote aliyehukumiwa adhabu hiyo kwenda kunyongwa.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, baada ya mahakama kumtia mtu hatiani na kumsomea adhabu ya kunyongwa mpaka kifo, mamlaka ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo inabidi kwanza yapate ridhaa ya kiongozi mkuu wa nchi, tena kwa kutia saini.
Mara ya mwisho kwa mfungwa kunyongwa ilikuwa mwaka 1994, enzi za utawala wa Rais wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi.
Baada ya Mwinyi akaja Rais Benjamin Mkapa ambaye akamwachia kijiti Jakaya Kikwete na wote hao hawakusaini mfungwa yeyote kunyongwa.
Mwaka 2017, Magufuli akiwa anamuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma alivunja ukimya juu ya suala hilo.
“Sisi wanasiasa tunaogopa kunyonga, natambua kwa sasa orodha ya watu ambao wanatakiwa kunyongwa ni kubwa sana, ila mimi naomba hiyo orodha msiniletee kwa sababu najua ugumu wake ulivyo,” alisema Rais Magufuli.
Hadi sasa mahakama za Tanzania zinaendelea kutoa adhabu hiyo kwa wale ambao wanakutwa na hatia kwa mashtaka stahiki.
Hukumu ya kifo duniani
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International hadi kufikia 2017 nchi 142 zimeacha kutoa hukumu ya kifo kisheria na/au kiutekelezaji.
Umoja wa Mataifa (UN) unakadiria kuwa nchi 170 zimeachana na adhabu hiyo kwa nman moja au nyengine.
UN ina wanachama 193, hivyo ni mataifa 23 tu ndio ambayo inawezekana walitoa hata hukumu moja ya kifo katika muongo uliopita.
JPM na Corona
Kuhusu virusi vya corona, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kutumia siku ya leo kuutafakari muungano ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume na kumuomba Mungu aepushe janga la corona.
“Rais Magufuli amewakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona (Covid-19) ikiwemo kujiepusha na mikusanyiko na safari zisizo za lazima,”ilisema taarifa hiyo ya Rais.
Aprili 22, akizungumza na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama mjini Chato, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu kwani si kila kifo kinachotokea kwa sasa kinasababishwa na corona na kuiiagiza wizara ya afya kutangaza takwimu za waliopona ugonjwa huo ili wananchi wajue.
Rais Magufuli pia alisema kuna baadhi ya watu wanashauri Jiji la Dar es Salaam lifungwe kwa kukataza watu kutoka nje ya nyumba zao, suala alilosema kamwe haliwezekani kwani jiji hilo ndilo kitovu cha biashara nchini.
“Si kila anayekufa ni corona ina maana malaria yameacha kuua, kuna upotoshaji mwingi umekuwa ukifanyika kwa ajili ya kuwatisha wananchi, kikubwa nawaomba Watanzania tuiondoe hofu kwa sababu hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko corona.
“Wanaotumia vibaya mitandao wajizuie katika kuandika uongo wa masuala ambayo hayapo, niwaombe pia wananchi muipuuze baadhi ya mitandao.
“Niviombe vyombo vya ulinzi na usalama IGP uko hapa shughulika nao hao ni saizi yako, shirikiana na TCRA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema Jiji la Dar es Salaam halitafungwa na kusisitiza watu waendelee kufanya kazi huku wakizingatia tahadhari zinazotolewa na wataalam.
“Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam hili haliwezekani, Dar es Salaam ndio ‘center’ pekee ambako collection ya revenue (makusanyo ya mapato) inapatikana.
“Sasa unapofunga ina maana wasipelekewe mchele, ndizi kutoka Bukoba, wasifanye biashara ya vitenge kupeleka vijijini, madereva wasibebe mafuta kupeleka mikoani.
“Unawazuia watu milioni sita ikitokea Mwanza, Mbeya nao utawafungia, utawafungia mikoa mingapi?” alihoji Rais Magufuli.
Pia alikemea dhana potofu iliyoanza kujitokeza kwa baadhi ya wananchi hasa waishio mikoani ya kuwatenga watu wanaotoka Dar es Salaam na kutaka ikomeshwe mara moja.
“Si kila anayetoka Dar es Salaam ana corona, dhana ya Watanzania kuwaogopa watu wa Dar es Salaama lazima iondoke, corona tutaishinda kwa ushirkiano, kwa kumaliza hofu, kwa kumtanguliza Mungu, kama tulivyoweza kushinda vita vingine,” alisema.