Na PATRICIA KIMELEMETA – Dar Es Salaam
RAIS wa Zambia, Edgar Lungu, amewataka watendaji wa Bandari Kavu ya Zambia (ZAMCARGO) na Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makasha Bandarini (TICTS), kuacha siasa na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kupata faida ambayo itachangia kukuza uchumi.
Akizungumza baada ya kukagua kampuni hizo zilizopo bandarini, Dar es Salaam jana, Rais Lungu alisema katika kipindi hiki ambacho nchi zinahitaji maendeleo, vitengo hivyo viwili vinapaswa kujikita katika shughuli za kukuza uchumi ili kuhakikisha wanafikia matarajio waliyokusudia.
Alisema muda wa kufanya siasa umekwisha kwa sababu wanasiasa wanakuja na kuondoka, lakini maendeleo yanabaki pale pale bila ya kuangalia chama.
Aidha aliziasa kampuni hizo kupanua wigo wa shughuli zao na kufanya kazi za ushindani, jambo ambalo linaweza kuchangia kuongeza mapato.
“Muda wa kufanya siasa umekwisha, kilichobaki ni kuchapa kazi ili kuhakikisha mnapata faida katika shughuli zenu, wanasiasa wanakuja na kuondoka, lakini maendeleo yatabaki pale pale,” alisema Lungu.
Aidha aliziasa menejimenti hizo mbili kukaa na kupanga mikakati mipya ambayo itawavutia wateja kufika kwenye ofisi zao kusafirisha mizigo, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza mapato.