RAIS Park Guen-hye wa Korea Kusini, amependekeza mabadiliko ya katiba ambayo yataondoa ukomo wa muhula mmoja wa urais na kumruhusu kiongozi kuhudumu mihula mingi.
Anataka ama mihula iongezwe au uanzishwe mfumo wa kibunge, akisema mfumo wa muhula mmoja wa urais umeshatimiza wajibu wake miaka 30 tangu uanzishwe.
Mabadiliko ya katiba ya mwaka 1987, yaliweka sharti la rais kuhudumu kwa muhula mmoja tu wa miaka mitano.
Kiongozi huyo anayeukosoa mfumo huo, alisema kipindi cha miaka mitano ni kifupi mno kuweza kuruhusu mwendelezo wa sera, ikiwamo ile ya kuziunganisha tena Korea mbili zilizotengana.
Park, ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa rais Korea Kusini, amebakiwa na miaka miwili kuhitimisha muhula wake Februari 2018.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) anayemaliza muda wake, Ban Ki-moon, alisema atarejea nyumbani nchini hapa, ambako wengi wanamshikiza kuwania urais.