NAIROBI, KENYA
MBUNGE mpya wa Igembe Kusini, John Paul Mwirigi ana kila sababu ya kutabasamu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumkabidhi gari aina ya Prado.
Gari hilo lilikuwa ahadi aliyokuwa ameahidiwa na Kenyatta iwapo Mwirigi angeshinda kiti hicho.
“Kazi imeanza na nakuhimiza uifanye kwa bidii,” Rais Kenyatta alimshauri Mwirigi alipomkabidhi funguo za gari hilo baada ya kukutana na wajumbe wa Mlima Kenya katika Ikulu ndogo iliyoko Sagana Lodge.
Akimkumbatia kwa furaha mbunge huyo alimuahidi Kenyatta  kuwa atatekeleza majukumu yake kama alivyowaahidi wananchi kabla ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.
“Ninakuahidi mheshimiwa Rais nitafanya kazi kwa bidii,” alisema Mwirigi (23), Â ambaye ndiye mbunge mdogo zaidi kiumri katika Bunge la 12.
Itakumbukwa mbunge huyo alikuwa akiendesha kampeni zake jimboni humo, takribani kilomita 200 mashariki mwa Nairobi, alikuwa akifadhiliwa na wasamaria wema wakiwamo waendesha boda boda na pikipiki.
“Katika kampeni zangu nilifadhaliwa na wasamaria wema wakiwamo waendesha bodaboda. Mafanikio yangu yametokana na neema ya Mungu, ninawashukuru walionichagua na kuniamini. Ninaahidi kuwafanyia kazi kwa uadilifu na uaminifu,” alisema.
Awali wabunge walipoalikwa Ikulu, alipewa lifti na mbunge mwenzake, lakini wakati wa kuondoka, alitumia usafiri wa umma maarufu kama matatu.
Mwirigi ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa ualimu katika Chuo Kikuu cha Mt. Kenya alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 18,867, akimshinda mpinzani wake wa karibu Rufus Miriti wa Chama cha Jubilee cha Rais Kenyatta, ambaye alipata kura 15,411.