Na Imani Nathaniel, Mtanzania Digital
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa China, Xie Xiaomao, kulipa faini ya Sh milioni 2 au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
Mshtakiwa huyo alikiri shtaka hilo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuhukumiwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imetaifisha kiasi cha zaidi ya Sh milioni 185 alizokutwa nazo mshtakiwa katika sehemu ya kubadilishia fedha, na sasa zimekuwa mali ya Serikali.
Katika hukumu yake, Hakimu Mushi alisema kuwa mshtakiwa amekiri shtaka hilo mwenyewe, hivyo mahakama inamhukumu kulipa faini ya Sh milioni 2, na endapo atashindwa, atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christine Joas, uliomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria na kutaifisha fedha alizokamatwa nazo mshtakiwa, ambazo ni Dola za Kimarekani 64,255 pamoja na Sh 16,797,000 za Kitanzania, kuwa mali ya serikali.
Kwa upande wake, wakili wa mshtakiwa, Mrisho Abdulhakim, aliomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa kuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, raia huyo wa China alitenda kosa hilo katika eneo la Supermarket ya Peninsula iliyopo Oysterbay, kati ya Januari 2024 hadi Mei 16, 2024. Mshtakiwa alidaiwa kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni ya Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na sheria.