MOSCOW, Urusi
RAIS Vladimir Putin wa Urusi, ameyataka mataifa yote duniani yanayomiliki kemikali kuiga mfano wa taifa lake ambalo limeteketeza silaha zote za maangamizi.
Taarifa ya Shirika la Habari la Urusi (TASS), jana ilimkariri wa Rais Putin akitoa raia hiyo alipokuwa akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) unaoendelea mjini The Hague, Uholanzi.
“Tunatoa wito kwa nchi ambazo zina silaha za kemikali kufuata mfano wetu na kufanya jitihada za kukamilisha hivi karibuni uondoaji wa zana zilizobaki zilizo nje ya mfumo wa kimataifa na wa kisheria wa mkataba huu kujiunga nao mara moja,” alisema Rais Putin.
Kwa mujibu wa Putin, shehena ya mwisho ya kemikali iliyokuwa ikimilikiwa na nchi hiyo iliteketezwa Septemba 27, mwaka huu jambo ambalo alisema ni hatua muhimu katika uwajibikaji na kuleta utangamano duniani.
“Nawahakikishia kuwa ushirikiano na mapenzi imara kisiasa yatasaidia kufikia lengo la kujenga ulimwengu bila silaha za kemikali,” alisema Rais Putin.
Mkutano huo wa 22 wa OPCW ulioanza Jumatatu wiki hii utamalizika kesho.