SOCHI, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, anatarajiwa kuwa miongoni mwa wageni mashuhuri watakaohudhuria droo ya mwisho ya kupanga ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia 2018 mji mkuu  Moscow, Urusi.
Droo hiyo iliyopangwa kufanyika wiki ijayo, inatarajiwa pia kuhudhuriwa na wanamichezo nguli pamoja na watu wengine maarufu duniani.
Taarifa iliyotolewa jana mjini Moscow na Msemaji wa Ikulu ya nchi hiyo, Dmitry Peskov, katika mahojiano na Shirika la Habari la nchi hiyo, TASS ambapo alisema kiongozi huyo kwa sasa anajaribu kupanga ratiba yake ili aweze kushiriki katika tukio hilo muhimu.
“Katika jambo hili kuna uwezekano mkubwa na tuna matumaini rais atapata muda wa kufanya hivyo,” Peskov aliwaambia waandishi wa habari na kuongeza kuwa upangaji wa ratiba ni tukio muhimu nchini humo kutokana na kwamba ni la kutafuta bingwa wa dunia.
Msemaji huyo wa rais alisema kwamba, kwa sasa maandalizi ya fainali hizo za mwaka yanakwenda vizuri na kwamba tukio hilo la upangaji ratiba litakuwa ni la aina yake.
Taarifa hiyo ya Ikulu imekuja siku mbili, baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kutangaza kwamba wanasoka nguli wa zamani wenye majina watahudhuria hafla hiyo ambayo imepangwa kufanyika Desemba mosi katika Ukumbi wa Ikulu ya nchi hiyo, State Kremlin Palace uliopo mjini Moscow.
Wachezaji hao ambao walitangazwa na Shirikisho la Kimataifa (Fifa) ni Laurent Blanc, Gordon Banks, Marcos de Morais (Cafu), Fabio Cannavaro, Diego Forlan, Diego Maradona, Carles Puyol, Miroslav Klose na Nikita Simonyan.