24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

PURA yalenga kuongeza matumizi ya nishati safi kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeweka malengo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi yafikie asilimia 80.

Akizungumza leo, Julai 12, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, alipotembelea banda la PURA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa, alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi unaoendelea nchini, wananchi wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia.

“Tunafanya tafiti mbalimbali ili kuwezesha jambo hili liwezekane kwa kuzalisha kiasi cha gesi ambacho kitaweza kuhudumia majumbani, katika magari, na kwenye maeneo mengine,” alisema Mhandisi Sangweni.

Alisisitiza umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira kama mkaa na kuni, na badala yake kutumia nishati safi ambayo haina madhara makubwa kwa mazingira. “Tumeweka malengo ya kutumia nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034,” aliongeza.

Kwa sasa, maeneo ambayo tayari yamegunduliwa kuwa na gesi ni pamoja na Mnazi Bay na Songosongo iliyopo Mtwara. Mhandisi Sangweni alieleza kuwa maeneo yenye viashiria vya mafuta yanajumuisha zaidi ya asilimia 50 ya eneo la Tanzania, ambapo tafiti zimefanyika katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 160,200, hasa katika maeneo ya Pwani.

Aliendelea kufafanua kuwa maeneo hayo ni Tanga, Kusini, na Mtwara, ambapo tafiti zimefanyika hadi baharini zaidi ya kilomita 400. Eneo hili tayari limepata kibali kutoka Umoja wa Mataifa (UN) na limeshagawanywa katika vitalu kwa ajili ya uwekezaji.

PURA inaendelea na ugunduzi katika maeneo ambayo yana viashiria vya gesi, na sasa wanatangaza maeneo mbalimbali ili kuvutia wawekezaji kushirikiana na taasisi pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) katika kutafuta na kuendeleza nishati hiyo.

“Shirika linaendelea na ugunduzi katika maeneo ambayo yana viashiria vya gesi ambapo imebainika kuwa ni asilimia 50 ya eneo la Tanzania,” aliongeza Mhandisi Sangweni. “Kwa sasa tunatangaza maeneo mbalimbali ambayo yanavutia wawekezaji kwa ajili ya kushirikiana na taasisi pamoja na TPDC katika kutafuta na kuendeleza kinachopatikana.”

Lengo la PURA ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi, hatua ambayo itaongeza usalama wa afya na kuboresha mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles