26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

PROFESA MUHONGO ANUSA RUSHWA KISIWANI KOME

prof-muhongo

Na BENJAMIN MASESE-SENGEREMA

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amebaini kuwa mafundi wa mkandarasi wa Wilaya ya  Sengerema mkoani Mwanza, huomba rushwa ili kuwaunganishia umeme wananchi wilayani humo.

Profesa Muhongo amebaini rushwa hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Kome chenye kata nne na vijiji 16 kilichopo wilayani Sengerema alipokwenda kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II).

Akiwa kisiwani hapo, wananchi walimweleza kuwa wamekuwa wakiombwa rushwa na mafundi wa mkandarasi wa Kampuni ya CHICO CCC anayetandaza waya wa umeme, kitendo ambacho kinawapa wakati mgumu kupata huduma hiyo.

“Tunashindwa kuelewa kauli za Serikali, maana tunaelezwa kuunganishiwa umeme kwa gharama ya Sh 27,000 lakini hapa mafundi wanatuomba kati ya Sh 50,000 hadi 100,000 ili kuunganishiwa umeme haraka, kibaya zaidi tunalazimika kukubali kwa sababu ofisi za Tanesco ziko mbali,” alisema Jaccob Masanja ambaye aliungwa mkono na wananchi wenzake.

Kutokana na malalamiko hayo, Profesa  Muhongo alipiga marufuku mafundi hao kuomba fedha kwani wao hawahusiki na suala la malipo huku akimuonya mkandarasi huyo na wengine nchini  ambao mafundi wake watabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa hatapewa miradi mingine.

Pia aliwaagiza viongozi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco)  mkoani Mwanza, kukutana na wananchi  mara moja na kukaa nao ili kutoa mafunzo sambamba na kuwatambua wanaohitaji umeme na kuwapatia huduma hiyo haraka.

“Nawaagiza viongozi wa Tanesco kuhakikisha wanakuwa na ofisi kwenye Kisiwa cha Kome wilayani Sengerema, anzeni taratibu za kuhamia hapa ili wananchi wasiendelee kutapeliwa,” alisema.

Profesa Muhongo alisema wananchi wa kisiwani humo hawapaswi kusumbuka kuvuka maji kufuata huduma kwenye ofisi za Tanesco ambazo zipo umbali mrefu.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO- CCC inayotekeleza mradi huo, Meck Nziku, alisema umeme uliosambazwa kisiwani humo ni wa kutoka katika Kijiji cha Nyakalilo kwa kutumia nyaya zinazopita chini ya maji (marine cable).

Aliongeza kuwa gharama zilizotumika kupitisha umeme huo chini ya maji ni Sh  milioni 200.

Akizungumzia suala la uunganishiwaji wa umeme kisiwani humo, Nziku alisema mradi huo ulilenga kuwaunganishia wananchi 718 lakini wananchi waliojitokeza kuunganishwa ni 579.

Hata hivyo, Profesa Muhongo aliwasisitiza wananchi kisiwani humo kuchangamkia mradi huo ikizingatiwa gharama ya kuunganishwa ni ndogo ambayo ni shilingi 27,000 sawa na bei ya majogoo wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles