23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Mkenda ataka mitaala ijibu mahitaji soko la ajira

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuendelea kufanya mapitio ya mitaala iliyopo ili kuendana na mabadiliko ya soko la ajira na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (Kulia), akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa, wakati alipokuwa akikagua mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Dar es Salaam.

Akizungumza leo Julai 18,2023 wakati wa kuzindua maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, amesema hatua hiyo itavifanya vyuo vikuu kuwa chachu ya maendeleo na suluhisho la changamoto mbalimbali.

“Kama taifa tunaendelea na mchakato wa mapitio na mageuzi makubwa ya mfumo wa elimu nchini, nchi yetu imeamua kufanya mageuzi makubwa ili kuwa na wahitimu wenye mtizamo chanya, maarifa na ujuzi zaidi kuweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe na kuchangia katika ujenzi wa taifa letu,” amesema Profesa Mkenda.

Pia ameitaka TCU kuongeza jitihada katika udhibiti wa ubora wa vyuo vikuu ili kuhakikisha lengo la kuwa na mitaala inayojibu mahitaji ya soko la ajira inatimia.

Kulingana na Profesa Mkenda, hadi kufikia Mei idadi ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya elimu ya juu ni 314,643 huku vyuo vikuu vilivyopo ni 32, vyuo vikuu 17 ambapo 19 vinamilikiwa na Serikali na 30 vya watu binafsi.

Aidha amesema maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya elimu ya juu yametokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ya ufundishaji na ujifunzaji.

Waziri huyo amesema pia mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka na kufikia Sh bilioni 652.7 kwa mwaka 2022/23 ambapo wanufaika ni 202,877.

Naye Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema maonesho hayo yameshirikisha taasisi 83 kutoka ndani na nje ya nchi ambapo zimeongezeka kutoka taasisi 75 za mwaka jana.

Amesema zaidi ya taasisi 20 zimekuja kupitia mawakala wanaopeleka wanafunzi nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Profesa Penina Mlama, amesema Serikali ipo kwenye mabadiliko ya mitaala na kwamba wataendelea kuchagiza vyuo vikuu kupokea mabadiliko hayo ili kuhakikisha vinaendelea kutoa elimu bora.

Kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inasema ‘Kukuza ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, sayansi na teknolojia kwa uchumi imara na shindani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles