Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Jamal Katundu amekitaka Chuo cha Maji kujikita kufanya tafiti zitakazotoa suluhisho la changamoto zilizopo katika sekta ya maji.
Akizungumza Novemba 2,2023 amesema upatikanaji wa maji nchini bado ni changamoto lakini chuo hicho kinaweza kuja na majibu. Alikuwa akizungumza wakati wa mahafali ya 47 ya Chuo cha Maji ambapo alimwakilisha Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
“Itakuwa ni kitu cha ajabu kama tuna mwalimu ana miaka sita hajawahi kufanya utafiti halafu anaendelea kufundisha watoto wetu, atakuwa anafundisha vitu vilivyopitwa na wakati ambavyo haviwezi kutatua changamoto tulizonazo.
“Tungependa kuona tafiti zenu zituambie kitu gani kinasababisha kuwepo na upotevu mkubwa wa maji, mtuambie vyanzo vipya vya maji…mkuu wa chuo tunategemea ripoti zako za mwaka utuambie tafiti mlizofanya na namna zilivyosaidia kutatua changamoto tulizonazo,” amesema Profesa Katundu.
Profesa Katundu pia ameagiza udahili unaofanywa uendane na ubora kwa kuhakikisha chuo hicho kinazalisha vijana wenye uwezo wa kutatua changamoto za maji.
“Wahitimu nchi hii inawahitaji, tunawategemea muwe sehemu ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya maji hivyo, ihudumieni nchi yenu,” amesema.
Mkuu wa chuo hicho, Dk. Adam Karia, amesema katika mwaka wa masomo wa 2023/2024 wameanzisha programu mpya nne na kufanya idadi ya programu kufikia 15 kutoka 11 za awali.
Aidha amesema wamedahili wanafunzi 2,197 ambalo ni ongezeko la asilimia 59 kutoka wanafunzi 1,384 wa mwaka 2022/2023.
“Chuo kinakua kwa kasi hivyo, ujenzi wa majengo na miundombinu unahitajika kukidhi ongezeko la wanafunzi,” amesema Dk. Karia.
Amesema pia wana programu ya kuwaendeleza watumishi kitaaluma ambapo watumishi 20 wako masomoni na kati yao 12 wanachukua Shahada ya Uzamivu, watano shahada ya uzamili na watatu shahada.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Felician Komu, amesema chuo kinatarajia kuanzisha programu mpya 13 katika mwaka ujao wa masomo ili kutoa wigo mpana wa kutatua changamoto za kisekta.
Katika mahafali hayo wahitimu 682 walihitimu katika ngazi za astashahada, stashahada na shahada huku waliofanya vizuri wakizawadiwa na wengine kupata fursa za ajira katika mamlaka mbalimbali za maji.