26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

TMA yatabiri mvua nyingi Novemba, Januari 2024

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua nyingi katika kipindi cha Novemba 2023 hadi Januari, 2024.

Akizungumza Oktoba 31,2023 na waandishi wa habari wakati wa kutoa mwelekeo wa mvua za msimu Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, amesema kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024).

Amesema mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro, Mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. Aidha, mvua za wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa kusini mwa Mkoa wa Katavi, Mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma.

Dk. Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), amesema uwepo wa El – Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu. Kuhusu hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pasifiki amesema linatarajiwa kuendelea kuwa la juu ya wastani katika kipindi cha Novemba, 2023 hadi Aprili, 2024.

“Hii inaashiria kuendelea kuwepo kwa hali ya El – Niño, hata hivyo, hali ya El – Niño inatarajiwa kupungua nguvu kadiri tunavyoelekea mwisho wa msimu wa mvua,” amesema Dk. Chang’a.

Kwa upande wa Bahari ya Hindi amesema hali ya joto la bahari la juu ya wastani inatarajiwa kuendelea kuwepo upande wa magharibi mwa bahari kwa msimu wote wa mvua za Novemba, 2023 hadi Aprili, 2024.

Mamlaka hiyo imewashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wakiwemo wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, mamlaka za maji na afya waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

Kuhusu mwenendo wa mvua za vuli mamlaka hiyo imesema zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles