Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, amemteua aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kumwakilisha katika mkutano wa makazi wa Habitat III unaofanyika katika mji wa Quito, Ecuador.
Taarifa aliyoituma kwenye mitandao ya jamii na Profesa Tibaijuka jana, ilisema katika msafara huo amefuatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi, Dk. Yamungu Kayandabila.
“Hivi sasa niko Geneva, Uswisi kwa matayarisho nikielekea Quito Ecuador mkutano wa makazi duniani wa HABITAT III kumwakilisha Rais wetu nikiwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,namshukuru Rais kwa heshima hii kubwa, Sitamuangusha.
Habitat III,ni mkutano wa uamuzi na mustakabali wa Shirika la Makazi Duniani na agenda ya maendeleo endelevu ya miji.
“Kama tunavyojua mkutano wa Habita I ulifanyika Vancouver,Canada mwaka 1976, Habitat II ulifanyika Istanbul, Uturuki mwaka 1996 na huu Ecuador Marekani ya Kusini 2016,”alisema.
Alisema kila baada ya miaka 20 wakuu wa nchi hukutana kukubaliana namna ya kuendeleza makazi kupitia Shirika la UNHABITAT ambalo aliwahi kuliongoza kwa miaka 10.
“Rais Magufuli alichaguliwa na kuongoza Baraza la Uongozi wa shirika hilo (Governing Council) kwa muhula wa mwaka 2006/2008 alipokuwa Waziri wa Ardhi.
“Wafanyakazi walimpenda kiasi kwamba alipobadilishwa wizara na kupelekwa Mifugo na Uvuvi karibu iwe zogo ofisini kwangu wakidai tutayumba.
“Niliwatuliza na kuwaambia kumbadilisha wizara hakumuondolei uenyekiti wake na kweli aliendelea nao na kumaliza,”alisema Tibaijuka.
Alisema katika mkutano huo, jambo kubwa akalolipigania ni utaratibu wa shirika hilo kuzisaidia nchi zinazoendelea kama sisi kwa kuzikopesha halmashauri zao fedha za miundombinu, bila kuilazimisha Serikali kuu kutoa dhamana kwa mikopo hiyo.
Alisema jambo hilo ni la msingi kwa vile huleta kasi ya maendeleo ingawa huwa linapingwa na wakubwa wanaotaka kukopa kupitia Serikali kuu ili waibane kwa kutumia Benki ya Dunia, kitendo ambacho kinachelewesha kasi ya maendeleo.
“Tutajitahidi kulingana na maelekezo ya Rais tunayemwakilisha kuhusu msimamo wa nchi yetu na washirika wake ambao ni nchi za Afrika na za G77 na China,” alisema.