29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Makubi aitaka mikoa jirani na Uganda kuchukua tahadhali na ya ebola

Na Clara Matimo, Mwanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ameitaka mikoa iliyo kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa ebola ikiwemo Kagera na  Mwanza, kuanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wanachi kupitia vyombo vya habari na matangazo ya mtaani ili kuhakikisha wanaelewa jinsi ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Prof. Makubi ametoa agizo hilo Septemba 29, 2022 alipokuwa mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi iliyolenga kujionea jinsi mkoa huo ulivyojipanga kusimamia mikakati ya kuzuia ugonjwa wa ebola ili usiingie nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi(kushoto) akijadiliana jambo na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda(kulia)pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa  huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa(kati kati).

Pia ameagiza uongozi wa mkoa huo kuimarisha na kuweka  mifumo ya maji  kwenye maeneo ya mkusanyiko ikiwemo stendi ili watu waweze kunawa mikono kwani ni njia mojawapo ya kupunguza ugonjwa wa ebola usisambae.

“Ukiosha mikono kama ambavyo tulikuwa na utaratibu huo wakati wa Uviko 19 itasaidia kuepusha ugonjwa huu hata kama kuna mtu  ambaye anamaambukizi lakini hajajitambua kuwaambukiza wengine maana si wote wanaoupata wana dalili za ugonjwa huo lakini wana uwezo wa kuambukiza, utaratibu wa kunawa mikono utasaidia pia kujikinga na ugonjwa wa  kovid 19, kipindupindu na  ebola.

“Uzuri wa huu ugonjwa hauambukizi kwa njia ya hewa  unaambukiza kupitia damu na vimelea vya majimaji kwa mtu ambaye ameishaambukizwa akimgusa ambaye hajaambukizwa na kuingia kwenye ngozi yake ambayo imechubuka hivyo hatuna budi kuhakikisha tunajikinga na kuwakinga wananchi wasiambukizwe njia nzuri ni kuwapa elimu.

Na nyie waandishi wa habari toeni elimu kwenye vyombo vyenu mbalimbali vya habari ili kuwaelimisha wananchi dalili za ugonjwa huo, jinsi ya kujikinga, unavyoambukiza na mtu akihisi dalili za ugonjwa huo afanye nini, wananchi wanaosafiri  nao watoe ushirikiano wa kupimwa ikiwemo wanaoingia hapa nchini kupitia uwanja wa ndege, stendi na bandarini,” alisema Profesa Makubi.

Aidha ameeleza kwamba  mkoa wa Mwanza umetenga jumla ya vituo 10 kwa ajili ya kuwatenga wagonjwa ambao watahitaji matibabu ya ugonjwa wa ebola endapo watabainika pamoja na kuwaweka kwa muda wale watakaotiliwa mashaka ya kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo na vifaa kwa ajili ya watumishi wa sekta ya afya ambao watawahudumia wagonjwa hao endapo watatokea.

“Lakini hatuombei mgonjwa atokee hapa nchini, hadi sasa nchi bado iko salama hatujawa na mgonjwa yoyote wa ugonjwa wa ebola usalama huo ambao upo tunahitaji uendelezwe  tunaweka mikakati ya kujikinga usiingie nchini maana hapa kuna mipaka ambayo mnapakana na mkoa wa Kagera ambao uko jirani na nchi ya Uganda ambako kuna wagonjwa wa ebola,”alisema.

Profesa makubi alitoa wito kwa  wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa yote nchini kuwa wasikivu kwa kufuata maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu wa afya wakubali kubadilika watambue kwamba zama hizi magonjwa ya mlipuko yanaweza kuibuka wakati wowote pia wakubali  kubadilisha tabia.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema wamejiandaa kwa ajili ya tiba na kinga ambapo wameanza kutoa elimu ya kinga kwa umma huku akifafanua kwamba kila halmashauri mkoani humo imeandaa kituo kwa ajili ya kutoa matibabu na kimewezeshwa vifaa tiba pamoja na wataalamu.

“Timu za wataalamu katika nyanja mbalimbali za afya wamepata mafunzo na zimejiandaa kwa ajili ya kutoa huduma endapo ugonjwa huo utaingia ndani ya mkoa huu  tunayo timu maalumu ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kutoa elimu ya afya kwa umma jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa ebola, unavyoambukiza na dalili za ugonjwa huoa ambapo pia  tumewashirikisha viongozi wa dini,”alisema Dk. Rutachunzibwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Utawala wa Mkoa wa Mwanza Daniel Machunda akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa huo Balandya Elikana alisema maelekezo yote yaliyotolewa na Wizara ya Afya watayatekeleza kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuanza mkakati wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.

“Tangu ugonjwa wa ebola ulipoingia nchi jirani ya Uganda na kutangazwa na wizara ya afya  tulianza kujipanga kwa kuweka mikakati ya kuzuia usiingie ndani ya mkoa wetu pamoja na kuandaa mazingira ya kuwatibu watakaobainika wana maambukizi endapo utaingia mkoani kwetu  maana mkoa wa Mwanza unapokea wageni wengi,”alisema Machunda.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ugonjwa wa ebola unaambukizwa kwa kugusa majimaji ya mwili kutoka kwa mtu mwenye maambukizi ya virusi vya ebola mfano matapishi, damu, jasho mkojo, mate, machozi na kamasi .

Dalili za ugonjwa huo  ni homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa maumivu ya mwili, misuli na viungo vya mwili, kuharisha kunakoweza kuambatana na damu, vipele mwilini, kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu mdomoni, puani, machoni na masikioni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles