NA SARAH MOSSI, UPPSALA
OKTOBA 20, mwaka huu, inatimia miaka 50 tangu wanafunzi wa iliyokuwa Dar es Salaam University College Mlimani sasa (Chuo Kikuu Dar es Salaam), walipoandamana kwenda Ikulu ya Dar es Salaam wakipinga Muswada wa Huduma ya Taifa ambao uliwataka kujiunga na Jeshi kwa miaka miwili na kutoa huduma bure kwa Taifa.
Maandamano hayo yalimkasirisha Mwalimu Nyerere na kwa mara ya kwanza aliamua kuwafukuza wanafunzi 400 pamoja na viongozi wao. Mwandishi wetu SARAH MOSSI alizungumza na Profesa Maalim Abdul-aziz Lodhi ambaye ni Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Uppsala nchini Sweden, anaelezea msingi wa maandamano hayo ambayo inaaminika ndiyo yaliyozaa Azimio la Arusha.
MTANZANIA: Uliwahi kuwa kiongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mlimani Dar es Salaam ambao walifukuzwa chuoni Oktoba 1966 hadi Mei 1967. Ni sababu zipi mliamua kupanga maandamano yaliyomkera Mwalimu Nyerere.
PROF. LODHI: Hili ni jambo kubwa sana. Siku zile hakukuwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kulikuwa na University of East Africa. Mwaka 1972 ndio wakavunja na kila nchi ikawa na chuo kikuu chake. Zaidi ya wanafunzi 400 walifukuzwa pamoja na viongozi wao lakini mimi peke yangu niliruhusiwa kurudi baada ya kuonekana sikuhusika kupanga maandamano yale.
Hii ilikuwa ni baada ya Serikali ikitaka kupitisha Muswada wa Huduma ya Taifa ambao ilikuwa ikiwataka wanafunzi kwenda jeshini miezi mitano kisha unafanya kazi yako miezi 18 halafu unarudi tena jeshini mwezi mmoja ndio unakamilisha miaka miwili.
Wakati unafanya kazi yako mwenyewe Serikali inachukua theluthi mbili ya mshahara wako kugharamia huduma ya Taifa. Maana ilikuwa ni sheria unapomaliza kidato cha sita au elimu ya juu ni lazima uende jeshini.
Mimi nikahoji wale waliomaliza kabla yetu na waliajiriwa na kupewa vyeo, maana siku zile dola ilikuwa ndio inapanuka kazi zilikuwa nyingi, unapomaliza tu unapewa kazi. Nikahoji ni kwanini hawa wasifanye huduma ya Taifa. Tukadai kila mmoja aende si sisi tu.
Lakini sisi wengine tulikuwa tumeshafanya huduma ya jeshi Tanzania Bara. Zanzibar kulikuwa hakuna huduma ya jeshi, kulikuwa na huduma ya jamii. Ndio maana mimi nilikwenda kufundisha kule Mkwajuni, Unguja miezi sita. Sasa kama tumefanya huduma ya jeshi au jamii tusilazimishwe kuingia tena jeshini.
Kama tumefanya mwaka mmoja huduma za jeshini au jamii basi twende mwaka mmoja huduma ya Taifa. Tusilazimishwe kwenda miaka miwili jeshini. Halafu tena kulikuwa na tatizo katika hii sheria. Zanzibar kule kulikuwa hakuna jeshi kulikuwa na Jeshi la kujitolea. Na hii sheria ilikuwa ya Tanzania Bara. Kulikuwa na majeshi mawili tofauti wakati ule Tanzania.
Kwa hiyo kwa sheria ya Zanzibar mimi kuingia jeshini Tanzania Bara nafanya kosa na naweza kutiwa ndani Zanzibar kwa wakati ule. Sasa niliposema hivyo wakakasirika. Na mimi nilikuwa ni mmoja wa wale wanafunzi wawili waliokuwa wakiwakilisha wanafunzi katika kamati ile ya Huduma ya Taifa.
Kulikuwa na Youth league wawili, Tanzania Parents Association (TAPA) wawili. Umoja wa wanawake wawili na kadhalika. Kwa hiyo mimi nilitoka Zanzibar na Charles Mwakasege wa Iringa. Kwa hiyo tulikuwa tunazungumza nao na kuwaeleza kwamba sisi tumekwenda jeshini.
Pia nilikwenda kuzungumza na marehemu Mzee Thabit Kombo, kwa urefu kabisa na akaniambia unachosema ni kweli lakini wengine hawakutaka kusikiliza.
Waliopanga maandamano ya kupinga walikuwa ni Dar es Salaam University College Student Union na waliandika risala yao waliyoiita Ultimatum to the Government, ndiyo Nyerere akakasirika sana maana yake Ultimatum unafanya Declaration of war na maana yake unatangaza vita.
Na hawakuwa wamepata kibali cha kufanya maandamano na kwa hiyo maandamano yale hayakuwa halali. Katika nchi nyingine wangepigwa risasi maana yake una-declare war.
Oktoba 22, mwaka huu tunaadhimisha miaka 50 ya maandamano yale. Lakini maandamano haya ndiyo yalisababisha kuharakishwa kuanzishwa kwa Azimio la Arusha.
Na kwanini Serikali ilichafuka wakati ule? Kwa sababu ilishindwa mara mbili kupitisha sheria ya Tanzania National Transport (TNT), Serikali ilitikisika na Bunge lilikataa kupitisha bajeti mara mbili na Nyerere akawatisha wasipokubali atalifunga Bunge. Na hii haimo katika Hansard, haikuchapishwa hadi leo.
MTANZANIA: Unasema hukushiriki katika maandamano yale na wewe ndiye ulikuwa ni kiongozi wa wanafunzi?
PROF. LODHI: Mimi sikushiriki nilikuwa ndiyo siku yangu ya mwisho kufanya Practice Aga Khan Secondary School nilikopelekwa. Lakini nilikwenda baadaye nikakuta wameshaingia Ikulu ndani.
Maandamano yalianzia Mnazi Mmoja na kuishia Ikulu. Na polisi na wanajeshi waliwaruhusu kufanya maandamno yale na kuwakaribisha waandamanaji Ikulu.
Mimi nilikwenda Ikulu ingawa nilikuta wameshaingia ndani, nikakutana na aliyekuwa Mkuu wa Huduma za Jeshi wakati ule Gama ambaye nilikuwa nafahamiana naye nilipokuwa Military Academy na mwanasiasa mmoja Songambele, wote watatu tukasimama na hapo milango ya Ikulu ikafungwa. Kwa hiyo tukakutana walioandamana na wasiofanya maandamano na mimi pia nikakamatwa.
Na siku ya pili picha ni moja tu iliyotoka Daily News ambayo ni picha yangu kwa sababu yule mpiga picha tulikuwa tunafahamiana.
Maandamano yale pia yalishuhudiwa na kina Samuel Sitta, Jaji Warioba na Sawe ingawa wao walisimama nje ya lango la Ikulu lakini wangethubutu kuingia ndani wangekamatwa pia.
MTANZANIA: Akina Sitta na Jaji Warioba nao walishiriki maandamano hayo?
PROF. LODHI: Hawakushiriki, wao walikuja kuangalia tu na kusikiliza hotuba ya mkuu wa Kilimani na Mwalimu.
MTANZANIA: Hebu tusimulie hotuba ya wanafunzi na Mwalimu zilisemaje?
PROF. LODHI: Kwanza ile hotuba ya wanafunzi iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza na katika kujibu hotuba ile ile Mwalimu alisema wametumia lugha ya mabwana zao na mimi nitawajibu kwa lugha ya mabwana zao. Na hotuba ile ya Mwalimu haijachapishwa kokote Tanzania lakini kwa Kiswidi kuna tafsiri yake.
MTANZANIA: Madai ya wanafunzi yalikuwa ni yapi katika risala yao kwa Mwalimu?
PROF. LODHI: Kama nilivyokwambia awali, wapunguziwe miaka ya kwenda huduma ya jeshi na kila mmoja aende na ndio maana Mwalimu kuanzia siku ile akaamua wabunge na mawaziri waende huduma ya jeshi japo wiki mbili au tatu na ndio maana akina Kawawa nao wakaenda jeshini na kuanza kuvaa nguo za kijeshi.
Na hapo hapo Mwalimu akatangaza kupunguza mishahara ya kila mmoja pamoja na mshahara wake nadhani alipunguza nusu ya mishahara. Kwa sababu ilikuwa watu wanapofanya huduma ya jeshi wanapewa theluthi moja tu ya mshahara ili kugharamia huduma yenyewe.
Lakini wale waliokwishapata kazi nzuri na vyeo walikuwa hawachangii kitu na walikwishapewa elimu bure na kwenda nchi za nje. Kwa hiyo watumishi wote wa Serikali walipunguziwa mishahara, sikumbuki ni asilimia ngapi.
Lakini pia wanafunzi walikuwa wanadai wanapofanya huduma za jeshi kama vile kufundisha si lazima kuvaa nguo za kijeshi na ilikuwa tupate posho ya Sh 180 na hata nguo za jeshi tufue sisi wenyewe. Sasa utaishije kwa posho ya Sh 180 kwa mwezi? Sasa mambo haya na mengine mengi yalikuwa yarekebishwe kabla ule Muswada haujapelekwa bungeni na jambo lingine tusamehewe mwaka mmoja kama tulishafanya huduma ya jamii au tusamehewe kabisa.
Simulizi hii ya maasi ya wanafunzi wa Mlimani ya mwaka 1966 kama ilivyosimuliwa na Prof. Lodhi itaendelea wiki ijayo…