33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Posho za Bunge kaa la moto

Bunge
Bunge

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

OFISI ya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za wajumbe wa Bunge hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge Maalumu, Jossey Mwakasiyuka, alisema ofisi ya Bunge hilo imekerwa na baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha taarifa hizo.

Alisema taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.

“Ni vema ikaeleweka kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato, na kwamba ujumbe wa Bunge Maalumu ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba mpya,” alisema Mwakasyuka.

Alisema si vizuri kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi yao vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalumu unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina na upatikanaji wa fedha toka benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika,” alisema Mwakasyuka.

Kutokana na hali hiyo, Mwakasyuka aliwataka wanahabari kuzingatia maadili na kanuni za uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao vya Bunge Maalumu.

“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles