25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WATAWANYA KWA MABOMU WALIOTAKA KUMWONA LOWASSA

Upendo Mosha na Elizabeth Hombo -Kilimanjaro/SINGIDA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya kundi kubwa la wananchi waliozuia msafara wa Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.

Maelfu ya wananchi hao walitawanywa jana kwa mabomu hayo baada ya kuziba barabara ya Soko la Mbuyuni eneo la Manyema wakati msafara wa Lowassa ukielekea Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basili Lema, alisema polisi walilazimika kurusha mabomu manne ya machozi ili kutawanya umati wa watu waliokuwa na shauku ya kumwona Lowassa.

“Saa 10:15 jioni katika Soko la Mbuyuni, polisi walirusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waweze kupisha msafara wa Lowassa kwa kuwa wengi wao waliziba kabisa barabara,” alisema.

Lema alisema kuwa Lowassa aliongozana na wabunge wawili wa chama hicho, Joshua Nasari na Esther Bulaya, kwenda kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Ninde Valerian.

Alisema baada ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kurusha mabomu hayo, wananchi walitawanyika na kuwezesha msafara huo kupita na kuelekea katika mkutano huo wa kampeni.

“Baada ya mabomu kurushwa, wananchi walitawanyika, tukaweza kuelekea katika mkutano wa hadhara na katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi Lowassa alihutubia,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, alithibitisha polisi kurusha mabomu hayo na alisema walifanya hivyo ili kutawanya umati wa wananchi waliokuwa wamefunga barabara katika eneo la Manyema.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema kama gharama za matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na kukimbizwa Hospitali ya Nairobi yakifikia Sh trilioni moja, wao wako tayari kuyagharamia hata kwa kuuza figo zao.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa chama hicho katika Kata ya Siuyu, Ikungi mkoani Singida, Gerald Mahami.

Lema alisema kutekeleza majukumu ya kisiasa wakiwa upinzani ni ngumu kutokana na kuwindwa kila siku.

Alisema pamoja na ugumu huo, hawatarudi nyuma na kisasi cha juhudi zao kimedhihirika kwa vitendo alivyotendewa Lissu.

“Lissu yupo kitandani, alipigwa risasi mwili mzima, gharama za matibabu yake ni kubwa, lakini hata ikifika shilingi trilioni moja na tukawa hatuna fedha, tutauza figo zetu kuendelea kugharamia matibabu yake kwa sababu Lissu amekuwa alama ya haki katika taifa letu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema leo watampokea aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, katika Uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles