27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI, KAGAME, SI MADIKTETA – PROF. LUMUMBA

Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


MWANAZUONI maarufu barani Afrika, Profesa Patrick Lumumba, amesema Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Rwanda, Paul Kagame si madikteta bali wanachokifanya ni kuhakikisha kunakuwa na siasa za miiko na maadili.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana katika Mkutano wa Pan African Humanitarian wa mwaka huu ulioandaliwa na Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa (Yuna) uliokuwa na kaulimbiu ya “amani inawezekana jana, sasa na kesho” na kuwakutanisha vijana kujadili nafasi zao katika kuleta amani barani Afrika.

Profesa Lumumba ambaye ni raia wa Kenya, alisema katika miaka ya hivi karibuni, wamekuja viongozi wenye mwelekeo na uchungu wa kuhakikisha mataifa yao yanaendelea, lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwaita madikteta.

“Tunapaswa kujua hawa watu tunaowaita madikteta ni akina nani, kwa sababu kuna viongozi wameibuka katika miaka mitatu hadi 20 iliyopita, wakiwa na mwelekeo na kuona uchungu wa kuhakikisha mataifa yao yanaendelea, lakini baadhi ya watu wengine wanawaita eti ni madikteta,” alisema na kuongeza:

“Lakini viongozi hao ni watu wazalendo na wakereketwa wa maendeleo endelevu, hivyo watu kama hawa lazima tujiulize mienendo yao ni ya kidikteta? Au ni ya kuhakikisha mataifa yao yanapiga hatua za haja na hoja. Mfano wengine wanasema Kagame, Dk. Magufuli ni dikteta, sikubaliani nao kwa sababu kile ambacho wanakifanya, wanajaribu kusema kwamba lazima kuwe na siasa za miiko na maadili.

“Nakubali kwamba udikteta ni jambo ambalo halistahili, lakini ni muhimu kuhoji kwamba uhuni ndiyo demokrasia? Kwa sababu kumeibuka wimbi la watu ambao ni wababaishaji hata sio wapinzani, kila kitu anachokifanya (rais) wao kazi yao ni kupinga.”

Akizungumzia suala la amani, hasa katika vipindi vya uchaguzi, alisema ni wakati wa kujiuliza ni aina gani ya uongozi inahitajika barani Afrika ili kuwe na njia ya kubadilisha uongozi isiyoleta vurugu tofauti na ilivyo sasa.

“Pia tunapaswa kuangalia hivi vitu tunavyoviita vyama, ni vyama kweli au ni vikundi tu, genge tu la vibarua waliokuja kujitafutia nyadhifa ili kupora mali za Waafrika. Vijana ndio wataibua hoja hii na kutathimini kuwa mataifa yetu tunayaandaa kwa minajili ya kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.

Pia alisema anaamini Afrika itakuja kuwa na amani na utulivu kwa sababu jitihada mahsusi zimeshaanza kufanywa na viongozi wake na tayari wamekwisha kutoa tamko kwamba kufikia mwaka 2020, lazima vitu vinavyoleta migogoro vitolewe na kila mtu anatakiwa kushiriki kwa nafasi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles