29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi watatu wapigwa bomu

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

NA AMON MTEGA, SONGEA

ASKARI polisi watatu wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kurushwa kwa mkono.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea juzi saa moja jioni katika Mtaa wa Mabatini wakati askari hao wakifanya doria.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa njiani kwenda mjini Songea, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mungulu, alikiri kutokea tukio hilo juzi.

“Ni kweli tukio hili limetokea saa moja jioni na hivi ninavyoongea na wewe hapa nimebakiza kilomita 100 kufika Songea mjini.

“Napata shida hata kutaja majina ya askari kwa sababu sijafika eneo la tukio, naomba uwe na subira nitawajulisha nikifika,” alisema DCI Mungulu.

Alisema kutokana na tukio hilo kutokuwa la kawaida, kikosi maalumu cha wataalamu wa mabomu kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kiliwasili mjini hapa kwa helkopta.

“Tumetuma kikosi maalumu cha wataalamu wetu wa mabomu, wao tayari wamewasili Songea, nategemea muda huu (jana jioni), wako eneo la tukio tayari,” alisema DCI Mungulu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, George Chipusi, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kusema hawezi kulizungumzia kwa kina.

“Tukio lipo ndugu yangu, siwezi kulizungumzia kwa kina kwa sababu nimepewa maelekezo kutoka ngazi za juu kuwa afande DCI ndiye atatoa taarifa rasmi ya tukio hili,” alisema Kamanda Chipusi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Daniel Malekela, amekiri kuwapokea askari hao na kusema wanaendelea na matibabu.

Alisema askari hao wamejeruhiwa sehemu mbalimbali ikiwamo miguuni na mbavuni.

Chanzo cha habari kutoka eneo la tukio, kimesema mmoja kati ya askari hao alifanikiwa kutoroka eneo la tukio na kukimbilia kwenye nyumba za wananchi kuomba nguo za kiraia.

“Askari aliyekuwa na bunduki alitumia ujanja wa hali ya juu, alitoroka hadi kwenye nyumba za jirani ambako aliomba apewe nguo za kiraia ili aweze kurudi kituoni,” kilisema chanzo chetu.

Tukio hilo limeonekana kuzua tafrani kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Songea. Hadi jana jioni eneo la tukio lilikuwa linalindwa na polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles