26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Polisi ‘wameza jiwe’ tuhuma za kumuua Dk. Slaa

kovaNA MWANDISHI WETU
MWENENDO wa uchunguzi dhidi ya madai ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kutaka kuuawa na mlinzi wake binafsi, Khalid Kangezi, umezua shaka.
Hii inatokana na ukimya wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambapo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa limeshindwa kuwahoji watuhumiwa waliotajwa na Dk. Slaa.
Gazeti hili limebaini kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ambao kwa pamoja wanashutumiwa kula njama ya kutaka kumzuru Dk. Slaa kwa kumshirikisha mlinzi binafsi wa kiongozi huyo wa Chadema, hawajahojiwa.
Si hivyo tu, Mchungaji Isack Loyd ambaye Kagenzi anamsukumia kuhusika na mipango hiyo, naye amesema hajapokea wito wowote wa Jeshi la Polisi kuhusu kuhojiwa.
Akizungumzia mwenendo wa kesi hiyo, Dk. Slaa aliliambia gazeti hili kuwa haridhishwi na jinsi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linavyoshughulikia kesi hiyo, hivyo alisisitiza kwamba hatokaa kimya kuzungumzia suala hilo.
Aliongeza kwa kusema kuwa amejaribu kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hatua zinazochukuliwa kuhusu kesi hiyo na kubaini kuwa viongozi wa CCM ambao wanadaiwa kula njama na mlinzi wake binafsi ili wazuru maisha yake bado hawajahojiwa.
“Si Mangula wala Kinana na hata huyo bwana Ngowi bado hawajahojiwa na Jeshi la Polisi na wakati mashahidi wote wameshahojiwa, ushahidi upo hata namba za mawasiliano ambazo waliwasiliana na mlinzi wangu tumewakabidhi ofsini kwao…lakini inasikitisha kuona watu walioendesha njama ya kutaka kuteketeza maisha yangu wanaendelea kuranda randa pasipo hatua yoyote kuchukuliwa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema amejaribu kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kesi hiyo na mara kadhaa Polisi wamekuwa wakimwambia kuwa faili la kesi hiyo bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
“Ninazo taarifa kuwa viongozi wa CCM wamekaa kikao cha kutaka kuzima kesi hiyo lakini nimesema sitokaa kimya…nimechoka kuvumilia vitendo vya namna hii, mwaka 2010 niliwekewa vinasa sauti chini ya kitanda changu lakini mpaka leo polisi hawajatoa ripoti yoyote ya uchunguzi waliouahidi,” alisema Dk. Slaa.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philip Mangula, ili athibitishe kama ameshahojiwa na Jeshi la Polisi au la, alishindwa kukataa wala kukubali badala yake alimwambia mwandishi kuwa yupo kwenye kikao na hata alipotafutwa Kinana simu yake haikupatikana.
Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova ambaye alijibu kuwa hafahamu chochote hivyo alimtaka mwandishi wa habari hii awasiliane na wasaidizi wake.
“Ngoja niulize wasaidizi wangu…Lakini kwanini umeniuliza swali hilo wakati sipo ofisini? Nitafute Jumatatu,” alijibu Kamishna Kova.
Madai ya kutaka kumzuru Dk. Slaa yaliibuka mapema Machi baada ya mlinzi wake binafsi, Kangezi kutekwa nyara na watu wanaotajwa kuwa ni makada wa chama hicho na kisha kumtesa kwa saa kadhaa kabla ya kwenda kumshtaki katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles